Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (Mb), Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitoa maelekezo ya namna ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 mapema leo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb).
Na: James Mwanamyoto - Dodoma
Tarehe 14 Juni, 2020
Taasisi za umma nchini zimeelekezwa kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 kwa kudumisha ushirikiano na wananchi na wadau, ili kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora kwa umma kwa kuzingatia Mikataba ya Huduma kwa Mteja.
Maelekezo hayo yametolewa mapema leo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (Mb), Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb).
Dkt. Mwanjelwa amesema, ushirikiano na wadau ni sehemu ya utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu ambayo inasisitiza jukumu la Utumishi wa Umma katika kujenga na kudumisha amani iliyopo miongoni mwa jamii.
“Katika mwendelezo wa kutekeleza Kauli Mbiu, naziagiza taasisi zote za umma kuadhimisha wiki hii kwa kufanya shughuli za kijamii katika maeneo ambayo wananchi wanapata huduma husani kwenye hospitali, masoko na maeneo mengineyo kwa kuzingatia tahadhari dhidi ya Corona, kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri yatakayowezesha utendaji kazi wa taasisi za umma.” Mhe. Mwanjelwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Watendaji wa Taasisi za Umma wanatakiwa kuadhimisha wiki hii kwa kukutana na watumishi katika maeneo yao ya kazi ili kusikiliza maoni na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa nje ili kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa, huku tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa CORONA zikichukuliwa.
Dkt. Mwanjelwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kutumia maadhimisho haya kujitathmini kama wanaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kwa dhati kuboresha huduma zitolewazo na Taasisi za Umma kwa wananchi na hatimaye kuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameziagiza Taasisi za Umma kuwasilisha taarifa ya namna walivyoshiriki maadhimisho hayo Ofisi ya Rais Utumishi mara baada ya kilele cha maadhimisho ili kuiwezesha Serikali kutumia taarifa hizo kufanya tathmini na kuboresha utendaji kazi.
Sanjali na hilo, amewapongeza Watumishi wote wa Umma kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo pamoja na changamoto za maambukizi ya Homa kali ya mapafu kuwepo.
Dkt. Mwanjelwa amewahakikishia Watumishi wa Umma kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inawathamini na iko pamoja nao, hivyo amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa manufaa na maendeleo ya taifa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anavyosisitiza kupitia kaulimbiu yake ya “HAPA KAZI TU” ambayo imekuwa ni chachu katika kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi kwenye Taasisi za Umma.
Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuanzia tarehe 16-23 Juni kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla. Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU) ni “Jukumu la Utumishi wa Umma katika Kujenga na Kudumisha Amani iliyopo Miongoni mwa Jamii.”
No comments:
Post a Comment