Tuesday, August 13, 2024

FCC MMECHOCHEA ONGEZEKO LA VIWANDA NCHINI-WAZIRI JAFO


WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo amesema Wizara hiyo ina fursa kubwa kutengeneza ajira kwa Watanzania kupitia sekta binafsi .

Amesema Sekta binafsi ni kwenye viwanda, hivyo watahakikisha wanatimiza azma hiyo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo kwa wanachi.

Waziri Dk.Jafo aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam, alipotembelea FCC kujitambulisha kwa viongozi wa Taasisi hiyo tangu ateuliwe na kuzungumza nao juu ya kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda ushindani wa soko nchini.

Alisema Wizara hii ni pana na ina umuhimu mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi kupitia sekta binafsi, hivyo lazima tuhakikishe mazingira mazuri kuongeza uwekezaji ambao unatoa ajira kwa Watanzania wengi na nchi kupata maendeleo

Alisema kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk.Samia, ndani ya miaka mitatu imechochea ongezeko la viwanda vikubwa kwa asilimia 27, ikiwa ni hatua kubwa ya ukuaji sekta hiyo na kuchochea ukuaji uchumi wa nchi pamoja na mtu mmoja moja kutokana ajira za viwanda vilivyojengwa na vinavyoendelea kujengwa.

Dk.Jafo Alisema kadiri iwezekanavyo watahakikisha wanaongeza kasi ya kutimiza azma ya Rais Dkt. Samia ya kuvutia uwekezaji kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Katika hatua nyingine, Waziri Dk.Jafo alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na FCC katika kuchochea ongezeko la viwanda kwa kuwezesha miungano halali ya viwanda vya ndani na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

"Mmefanya kazi nzuri iliyowezesha serikali kupata mabilioni ya fedha, mpendane, mshirikine katika kufanya kazi kwa bidiii ya kuendeleza kazi hii muhimu pamoja na kushirikiana kufanya ukaguzi kwa kampuni mbalimbali ikiwemo ya madini ambayo yameungana bila kufuata taratibu.

Nae Mkuu wa FCC, William Erio, alimshukuru Waziri Dk. Jafo kwa ziara hiyo katika ofisi zao, huku akisema wako tayari kushirikiana naye kutimiza azma ya serikali.

Alisema FCC inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha ushindani halali nchini, kudhibiti bidhaa bandia, kwa lengo la kulinda soko na kuvutia uwekezaji kwa uwepo mazingira bora ya biashara nchini.

Alisema katika kutekeleza hilo wamewezesha maboresho ya sheria kuendana na mazingira ya sasa, hali ambayo imesaidia katika kuwezesha muungano wa kampuni na viwanda, ambavyo vimechochea ukuaji na uwekezaji nchini na kukuza uchumi.

No comments: