Thursday, August 8, 2024

WANANCHI ILEMELA WATAKIWA KUIUNGA MKONO TIMU YA PAMBA JIJI

Wananchi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela wametakiwa kuiunga mkono timu ya mpira wa miguu ya Pamba Jiji ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya ligi kuu ya Tanzania bara

Hayo yamesemwa na mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Ilemela ambae pia ni Katibu tawala wa wilaya hiyo Wakili Bi Mariam Abubakar Msengi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa tawi la timu hiyo katika viwanja vya stendi ya daladala Pasiansi ambapo akawataka kuhakikisha wanajitoa kwa hali na mali kuunga mkono harakati zote zotakazochangia timu hiyo kufanya vizuri katika ligi kuu ya mpira wa miguu

‘.. Uzinduzi wa tawi hili uende sambamba na uungwaji mkono kwa timu yetu, Hii ndio timu ya wana Ilemela, hii ndio timu ya kanda ya ziwa, hii ndio timu yetu watu wa Mwanza ..’ Alisema

Aidha Wakili Msengi akamshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa juhudi zake za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na mpango wake wa ukarabati wa uwanja wa mpira wa miguu wa CCM Kirumba kwaajili ya matumizi ya mashindano ya AFCON na ujenzi wa kituo kipya cha michezo kata ya Buswelu


Kwa upande wake afisa michezo Jiji la Mwanza ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya uhamasishaji Ndugu Mohamed Bitegeko akafafanua kuwa timu ya Pamba Jiji inaendesha kampeni ya kuhamasisha wananchi kununua jezi kwa thamani ya shilingi elfu thelathini na ununuzi wa tiketi kwa madaraja tofauti tofauti ili kuisaidia timu hiyo kiuchumi na kuleta hamasa kwa wananchi ili kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali

Nae mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu akaongeza kuwa manispaa yake itaendelea kushirikiana na uongozi wa timu hiyo ili kuisaidia kufikia malengo yake pamoja na kuahidi kununua tiketi kwaajili ya madiwani na watumishi wa manispaa ili waweze kushiriki sherehe za siku ya timu ya mpira wa miguu ya Pamba Agosti 10, mwaka huu

Uzinduzi wa tawi hilo ulienda sambamba na ukaguzi wa kikosi cha timu ya mpira wa miguu ya walimu wanaume itakayoshiriki mashindano ya shirikisho la michezo la watumishi wa Serikali za mitaa (shimisemita)

No comments: