ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 23, 2026

WATUHUMIWA WA KUSAFIRISHA KILO 20.03 ZA SKANKA KATIKA BASI LA KING MASAI TOURS WASOMEWA MASHTAKA

WATUHUMIWA wawili, Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza, Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji,  Januari 22, 2026, wamefikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke kujibu tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya skanka.

Akisoma maelezo ya awali ya shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Lukosi, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Wakili Nicas Kihembe akisaidiana na Erick alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa tarehe 08 Desemba 2025 katika mtaa wa Wailes, Temeke, Dar es Salaam na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), wakihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Ilidaiwa mahakamani hapo  kuwa, wakati wa operesheni hiyo, DCEA ilikamata pakiti 20 za Bangi aina ya  skanka zenye uzito wa jumla wa kilogramu 20.03, ambazo zilikuwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba, kisha kufichwa katika basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili wa Msumbiji AAM 297 CA.

Ilielezwa zaidi kuwa, mashtaka yanayowakabili washtakiwa ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 16(I) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inayokataza umiliki, usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya nchini.

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa, shtaka hilo halina dhamana kutokana na uzito wa dawa za kulevya walizokutwa nazo washtakiwa.


Aidha, kwa mujibu wa wakili wa Serikali, upelelezi wa shauri hilo  namba 1535/2026 ya mwaka 2026 bado unaendelea na mashahidi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo siku itakayopangwa.

Shauri hili  lilihairishwa  hadi tarehe 05 februari 2026, huku washtakiwa wakirejeshwa rumande.

Mwisho

No comments: