Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, amezungumza na viongozi wapya wa Chama cha Watanzania Waishio Ufaransa (Diaspora Tanzania France) kujadili nafasi ya diaspora katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza na viongozi hao katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris, Balozi Yakubu amewapongeza kwa kuaminiwa kuongoza jumuiya hiyo na kusisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wa diaspora katika maendeleo ya taifa. Amesema utaalamu na uzoefu wa Watanzania waishio nje ya nchi ni rasilimali muhimu katika kukuza uwekezaji, biashara, utalii na uhamishaji wa maarifa.
Aidha, Balozi Yakubu amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ushiriki wa diaspora katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Pia amewahimiza kutumia nafasi zao za kitaaluma, kijamii na kiuchumi kuitangaza Tanzania kimataifa, sambamba na kuhamasisha fursa za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo nchini.
Vilevile, amesema Ubalozi utaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na diaspora katika kuimarisha mawasiliano, uratibu na ushirikiano wenye tija. Ameongeza kuwa Ubalozi utaendelea kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili na kuitangaza Tanzania katika nchi zote zilizo chini ya eneo lake la uwakilishi ambazo ni Ufaransa, Hispania, Ureno na Morocco.
Kwa upande wao, viongozi wa Diaspora Tanzania France wameeleza dhamira yao ya kuimarisha mshikamano wa Watanzania wanaoishi Ufaransa, kuendeleza matumizi na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili, pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali nchini Tanzania katika sekta za maendeleo, elimu, teknolojia na uwekezaji.
Viongozi hao, ambao ni wataalamu katika fani mbalimbali zikiwemo sayansi ya nyuklia, akili mnemba (AI), jiolojia, teknolojia na utafiti, wameahidi kutumia utaalamu na uzoefu wao kuchangia maendeleo ya Tanzania kupitia ushauri wa kitaalamu, uhamishaji wa maarifa na ushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo.



No comments:
Post a Comment