ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 5, 2026

DKT. ART ULENE KUSHEREHEKEA MIAKA 90 JUU YA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO

 


Na. Calvin Katera - Kilimanjaro


Dkt. Art Ulene, Daktari mstaafu kutoka  nchini Marekani na aliyewahi kuwa mwandishi wa masuala ya afya wa kituo cha televisheni cha NBC, ameanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuvunja rekodi ya kuwa mtu wa kwanza mwenye umri wa miaka 90 kukwea hadi katika kilele cha Uhuru chenye mita 5895 kutoka usawa wa bahari. 

Kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na raia wa Marekani anayeitwa Anne Lorimor, aliyepanda Mlima Kilimanjaro akiwa na umri wa miaka 89 na siku 37, akipandia lango hilo hilo la Rongai Julai 18, 2019 na kufanikiwa kufika katika kilele hicho ambacho kinavutia kwa macho kutokana na uwepo wa mrundikao wa barafu.

Safari  hiyo ya Dkt.  Ulene ya kuvunja rekodi ya Bi. Lorimor ilianza Julai 03, 2026 katika Lango la Rongai iyotarqjiwa kuchukua siku 10 ameilekeza katika kumbukizi yake ya kuzaliwa inayosherehekewa kila ifiapo Julai 13, siku anayoitarajia imkute akiwa katika kilele kirefu kuzidi vyote barani Afrika, huku akitimiza ndoto yake kuvunja rekodi hiyo iliyodumu kwa takribani miaka saba. 

Akizungumza kabla ya kuanza safari hiyo, Dkt. Ulene alisema wazo la kurejea Kilimanjaro lilianza kama mzaha kati yake na marafiki, lakini baadaye likageuka kuwa safari yenye maana kubwa ya kujipima uwezo na kuhamasisha watu kutokukata tamaa kutokana na umri.

Alisema baada ya kuupanda Mlima Kilimanjaro mara tatu zilizopita, ameendelea kuvutiwa na uzuri wa mlima huo pamoja na ukarimu wa Watanzania. Kwa mujibu wake, Mlima Kilimanjaro ni mfano wa maisha yenye changamoto na mafanikio, huku akisisitiza kuwa safari hiyo si ya kuvunja rekodi pekee bali ni ya kujitambua na kuthibitisha uwezo wa binadamu.

Dkt. Ulene alisema umri unaweza kufanya mambo kuwa magumu zaidi, lakini haupaswi kuwa kikwazo cha kutimiza ndoto. Amehimiza watu kuendelea kufuata malengo yao, akieleza kuwa kila mmoja ana "mlima wake” wa kupanda katika maisha.

Aliongeza kuwa akifanikiwa kufika katika Kilele cha Uhuru, atasherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 90 pamoja na timu yake kwa keki na nyimbo za kumbukumbu. Hata hivyo, amekiri kuwa bado anaiheshimu changamoto ya Mlima Kilimanjaro, hususan baridi na upepo mkali unapofikia zaidi ya mita 3700 kutoka usawa wa bahari.

Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza, Hifadhi ya Taifa  Kilimanjaro, Hilda Mikongoti, alisema kuwa safari hiyo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania na Mlima Kilimanjaro duniani sanjari na kurejea kwa Dkt. Ulene kwa mara ya nne ni uthibitisho wa ubora wa huduma zinazotolewa na hifadhi hiyo.

Muhifadhi Mikongoti aliongeza, “KINAPA imefanya maandalizi ya kutosha kwa kushirikiana na Kampuni ya World Wild Travel Tanzania inayompandisha Dkt. Ulene, ikiwemo kuongeza muda wa safari hadi siku 10 ili kumpa nafasi ya kuzoea mabadiliko ya mwinuko na kuhakikisha anafika kileleni.”

Aidha, alisisitiza kuwa Mlima Kilimanjaro unaweza kupandwa na mtu yeyote mwenye maandalizi sahihi, akibainisha kuwa hata wenzetu wenye mahitaji maalumu wamewahi kufika kileleni kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu na huduma ndani ya hifadhi.

Naye Mkurugenzi wa World Wild Travel Tanzania, Raymond Maasai, alisema maandalizi ya safari hiyo yalianza mwaka jana, huku ratiba maalumu ikiandaliwa ili kumpa Dkt. Ulene muda wa kutosha wa kupanda taratibu, kupumzika mara kwa mara na kutumia vifaa maalumu vinavyoongeza faraja wakati wote wa safari.

Wadau wa utalii wanaamini kuwa mafanikio ya Dkt. Ulene yataongeza umaarufu wa Mlima Kilimanjaro katika soko la utalii duniani na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utalii wa milima, huku yakibeba ujumbe kwamba ndoto hazina umri na zinaweza kutimizwa kwa maandalizi sahihi, dhamira na ujasiri.










No comments: