Na Mwandishi Wetu, Lindi
LINDI: Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar K. Mmuya, ametembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yanayoendelea Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi, na kujionea teknolojia na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na TFS katika uhifadhi wa rasilimali za misitu.
Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Agosti 4, 2026, Mmuya alijionea matumizi ya teknolojia ya drone katika uhifadhi wa misitu, shamba darasa la miti, elimu na fursa za ufugaji wa nyuki pamoja na bidhaa na huduma zinazotokana na mazao ya misitu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Manyisye K. Mpokigwa, ambaye ni Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini, alisema banda hilo pia limewakutanisha wadau mbalimbali wa mazao ya misitu wakiwemo wajasiriamali wa vikapu, watengenezaji wa samani za ndani kama vitanda na milango, pamoja na wauza maua na miche ya matunda.
Alisema ushiriki wa wadau hao unalenga kuwaonesha wananchi na washiriki wa maonesho fursa zilizopo katika sekta ya misitu, huku ukihamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa ajili ya kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alipata fursa ya kukata keki na kuonja asali safi inayozalishwa na wafugaji nyuki wanaoshirikiana na TFS kabla ya kukabidhiwa zawadi ya Asali ya Nyuki Wadogo na Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Manyisye K. Mpokigwa.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yanaendelea Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi, yakibeba kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko: Ongeza Tija Kutekeleza Dira ya 2050,” huku yakitarajiwa kuendelea kuvutia washiriki na wadau kutoka sekta mbalimbali za uzalishaji nchini.






No comments:
Post a Comment