Na Mwandishi Wetu, Dole Kizimbani, Zanzibar
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeandika historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza Maonesho ya Kilimo Zanzibar, hatua iliyopokelewa kwa pongezi na viongozi pamoja na wananchi kutokana na kupeleka elimu na fursa za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi wa misitu na nyuki visiwani humo.
Mafanikio hayo yalidhihirika Agosti 5, 2026, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Haroun Ally Suleiman, kutembelea banda la TFS katika Viwanja vya Dole, Kizimbani na kupongeza uamuzi wa wakala huo kuvuka bahari na kuwaletea Wazanzibari huduma za elimu ya uhifadhi pamoja na fursa za uwekezaji.
"Niwapongeze sana TFS kwa kuona umuhimu wa kutangaza fursa za uhifadhi hapa Zanzibar. Ni hatua nzuri ambayo itawanufaisha wananchi kwa kuwawezesha kuibua vyanzo vipya vya mapato kupitia uhifadhi wa misitu," alisema Waziri Haroun.
Alisema ushiriki wa TFS katika maonesho hayo unafungua milango mipya ya ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika kukuza uchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki, huku akiitaka taasisi hiyo kuendelea kushiriki maonesho na kampeni za uelimishaji visiwani humo.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Francis Kiondo, alisema ushiriki huo wa kwanza Zanzibar ni sehemu ya mkakati wa TFS wa kusogeza huduma karibu na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhakikisha fursa za uhifadhi zinawafikia Watanzania bila kujali walipo.
Alisema kupitia maonesho hayo, wananchi wanapata elimu kuhusu uhifadhi wa misitu na nyuki, uzalishaji wa mbegu bora za miti na miche, ufugaji nyuki, fursa za uwekezaji katika sekta ya misitu pamoja na utalii wa ikolojia, ambao unazidi kuwa chanzo muhimu cha ajira na mapato.
Maonesho ya Kilimo Zanzibar yanaendelea katika Viwanja vya Dole, Kizimbani kuanzia Agosti 1 hadi 14, 2026, ambapo TFS imewahimiza wananchi kutembelea banda lake ili kujifunza na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu.

No comments:
Post a Comment