Friday, February 12, 2010

Kakobe agomea kikao na Waziri Ngeleja!

Sakata la Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship , Zacharia Kakobe na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeingia hatua mpya baada ya kiongozi huyo kukataa wito wa kufanya kikao kesho na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutokana na kile alichodai, ufisadi wa vipimo uliofanywa na taasisi iliyopewa kazi hiyo.

Akizungumzia hilo,Askofu Kakobe alisema taasisi iliyopewa kazi hiyo ya Bureau for Industrial Cooperation (BICO) ilibadili vipimo na kuandika visivyo kwa lengo la kuihalalisha TANESCO iweze kutandaza umeme katika eneo lake.

“Siwezi kuhudhuria kikao cha kesho na Waziri Ngeleja kwa kuwa wale waliofanya uhuni huu watakuwepo na Askofu yeyote hawezi kukaa meza moja na wahuni, hivyo sitakwenda. Namuomba Rais Jakaya Kikwete aingilie mzozo huo.” alisema Kakobe.

Alisema hivi sasa hakuna asiyejua kwamba kuna makundi ya kisiasa yanayotaka kumchafua rais na wanataka kutumia nafasi hiyo kutugombanisha mimi na waumini ili tuichukie serikali ya Kikwete lakini ukweli ni kwamba Rais Kikwete ni muadilifu na atachukua hatua kwa kuwa hawa waliopewa jukumu hili wanaonesha wazi kuwa wana nia ya kuleta vurugu za kidini hapa nchini.

No comments: