Monday, February 8, 2010

Mbongo aliyeuawa India azikwa bila kichwa!


Vilio, simanzi na majonzi jana vilitawala mazishi ya Mtanzania Imran Mtui (31) aliyeuawa kikatili nchini India hivi karibuni, katika mazishi yaliyofanyika makaburi ya Njoro Manispaa ya Moshi.

Hata hivyo mwili huo ulizikwa bila kichwa huku pia ukidaiwa kuwa na majeraha mengi mwilini kuanzia miguuni na kwenye paja lake karibu na kiuno huku kiwiko cha mkono wa kulia nacho kikidaiwa kunyofolewa.

Mwili huo uliwasili mjini moshi usiku wa kuamkia jana baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam, ukitokea nchini India huku gharama zote za kuusafirisha zikibebwa na serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, mwili huo pia umeonekana kuwa na alama za kamba kwenye mikono yake hali ambayo inaonyesha marehemu kabla ya kuuawa alifungwa kamba ili asiweze kujitetea.

Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea katika mji wa Bangalore nchini India ambako marehemu alikuwa tayari amehitimu masomo yake ya biashara na utawala (Business Administration) na tayari alikuwa akijiandaa kurejea nyumbani.

Kaka huyo wa marehemu aliwaambia waandishi wa habari kuwa mdogo wake huyo alipatwa na mkasa huo akiwa njiani kuelekea mjini ambako rafiki yake wa kike ambaye pia ni Mtanzania aishie visiwani Zanzibar alikuwa akisoma.

No comments: