Na Theonestina Juma, Bukoba
ZIKIWA zimebaki siku 10, kabla masalia ya mwili wa aliyekuwa Kadinali wa kwanza mweusi barani Afrika, Laurean Rugambwa, kuzikwa upya kwenye Kanisa Katoliki la kwanza mkoani Kagera, uongozi wa kanisa hilo umetoa onyo kali kwa wafanyabiashara walioanza kunufaika na tukio hilo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba, kutengeneza fulana zenye nembo ya kanisa hilo na picha ya Kadinali Rugambwa, ambazo zinauzwa sh. 12,000 bila ridhaa ya uongozi wa kanisa hilo.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Padri Deodatus Rwehumbiza, alisema waumini ambao watanunua fulana zilizotengenezwa na wanyabiashara hao bila baraka za kanisa hilo, watakuwa wamefanya makosa.
“Upo utaratibu ambao umeandaliwa na kanisa kwa kukaa katika maeneo maalumu yaliyotengwa, waumini ambao watavaa fulani zinazouzwa na wafanyabiashara hawatapewa kipaumbele kwa sababu si zale za tukio lililopo mbele yetu.
“Zipo sare ambazo zimeandaliwa ili waumini ambao watahudhuria tukio hili waweze kufahamika kirahisi, wanaponunua sare zetu wanachangia ufanisi wa sherehe hizi,” alisema.
Padri Rwehumbiza alitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti hili kutaka kujua kama waumini hao watakwenda kanisani siku hiyo wakiwa na sare walizozinunua kwa wafanyabiashara bila ridhaa ya uongozi wa kanisa hilo watafanyaje.
“Masalia ya mwili huu yatahamishwa Agosti 6-7 mwaka huu, kutoka kwenye Kanisa la Kashozi alilozikwa kwa muda,” alisema.
No comments:
Post a Comment