Advertisements

Wednesday, October 3, 2012

Ni SIMBA NA YANGA LEO, KAZI IPO TAIFA

Mechi iliyopita...5-0

VIKOSI VYA LEO:
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Edward Christopher, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Mrisho Ngassa.
BENCHI: Wilbert Mweta, Komabil Keta, Paschal Ochieng, Kiggi Makassy, Salum Kinje, Daniel Akuffo, Abdallah Juma na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
KOCHA; Milovan Cirkovick (Serbia)
Yanga SC

YANGA: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Cannavaro, Kevin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.
BENCHI: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Godfrey Taita, Stafano Mwasyika, Job Ibrahim, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Shamte Ally, Idrisa Rajab na Jerry Tegete. 
KOCHA; Freddy Minziro
Simba SC

Na Mahmoud Zubeiry
WATANI wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga wanashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini, kuanzia saa 11:00 jioni.
Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-0 katika mchezo uliopita Mei 6, mwaka huu dhidi ya wapinzani hao wa jadi.
Aidha, Simba inaingia kwenye mchezo wa leo, ikiwa inaongoza Ligi, baada ya kushinda mechi zake zote nne na kuvuna pointi 12, wakati Yanga inashika nafasi ya tano kwa pointi zake saba, zilizotokana na sare moja, kufungwa mechi moja na kushinda mbili katika mechi nne ilizocheza.
Simba inatokea Zanzibar ilipoweka kambi kwa zaidi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo, wakati Yanga wanatokea hapa hapa Dar es Salaam, Double Tree By Hilton, walipoingia Jumapili usiku wakitokea Uplands, Changanyikeni walipoanzia kuweka kambi yao. 
Simba leo itawakosa beki wake Amir Maftah na mshambuliaji wake Emmanuel Okwi, ambao wanatumikia adhabu za kadi nyekundu, wakati Yanga ina majeruhi mmoja tu na wa muda mrefu, Salum Telela.
Hapana shaka, Mserbia Milovan Cirkovick ataendelea kuwapanga pamoja Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ na Felix Sunzu katikati na Mrisho Ngassa na Edward Christopher watashambulia kutokea pembeni.
Yanga kadhalika- kuna uwezekano Freddy Felix Minziro akawatumia Didier Kavumbangu na Said Bahanuzi katikati na Hamisi Kiiza na Simon Msuva watashambulia kutokea pembeni.
Haruna Niyonzima katika kiungo cha Yanga na Mwinyi Kazimoto katika kiungo cha Simba ni burudani nzuri inayotarajiwa Taifa leo.
Amri Kiemba atacheza kama kiungo wa ulinzi upande wa Simba, wakati kwa Yanga bila shaka atakuwa Athumani Iddi ‘Chuji’.
Beki wa kulia wa Yanga atakuwa Juma Abdul au Mbuyu Twite, wakati kushoto atakuwapo Oscar Joshua au Mbuyu hata Stefano Mwasyika.
Beki wa kulia wa Simba bila shaka atakuwa Nassor Masoud ‘Chollo’ na kushoto atakuwa Paul Ngalema, au Kiggi Makassy.
Katikati Yanga, Minziro anaweza kuamua kumpanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan na haitakuwa ajabu pia Twite akimuweka benchi mmojawao.
Simba hapana shaka Milovan ataendelea kuwachezesha pamoja katikati Shomary Kapombe na Juma Nyosso. Langoni Simba piga, ua atasimama Kaseja tu labda awe mgonjwa wa kushindwa kucheza hata kwa sindano ya ganzi. Yanga bila shaka atadaka Mghana Yawe Berko. 


JE WAJUA?
1.Mara ya mwisho Simba na Yanga kukutana ilikuwa ni Mei 6, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Wekundu wa Msimbazi walishinda 5-0, mabao ya yakifungwa na Emmanuel Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na Patrick Mafisango (penalti dk 72).
2.Pambano la kwanza la Ligi Kuu, wakati huo klabu ya bingwa ya taifa baina ya watani wa jadi lilifanyika Juni 7, mwaka 1965 Uwanja wa Ilala (sasa Karume), wakati huo Simba bado inaitwa Sunderland na Yanga ndio walioshinda mechi hiyo, bao pekee la Mawazo Shomvi dakika ya 15.
3.Ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ni wa mabao 5-0 Juni 1, 1968, siku hiyo Maulid Dilunga ‘Mexico’ akifunga mabao mawili katika dakika ya 18 kwa penalti na na 43, wakati mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 na Kitwana Manara dakika ya 86.
4.Ushindi mkubwa kwa Simba dhidi ya Yanga ulikuja Julai 19, mwaka 1977, mabao 6-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- siku hiyo Abdallah ‘King’ Kibadeni akifunga mabao matatu peke yake katika dakika za 10, 42 na 89 wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na beki wa Yanga, Suleiman Sanga akajifunga dakika ya 20.
5.Sare ya mabao 4-4 Novemba 9, mwaka 1996 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, inabakia kuwa sare ya kihistoria katika mapambano ya watani wa jadi kufungana mabao mengi. Mabao ya Yanga yalifungwa na Edibilly Lunyamila kwa penalti dakika ya 28, Mustafa Hozza alijifunga dakika ya 64, Said Mwamba 'Kizota' dakika ya 70 na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ dakika ya 75. Simba mabao yao yalifungwa na Thomas Kipese dakika ya saba, Ahmed Mwinyimkuu dakika ya 43 na Dua Saidi dakika ya 60 na 90.
6.Leo Yanga inatarajiwa kuongozwa na kocha mzalendo, beki wake wa zamani Freddy Felix Minziro wakati Simba ina Mserbia, Milovan Cirkovic- hii ni mara ya pili mfululizo benchi la Yanga kuwa na kocha mzawa katika mechi dhidi ya watani, kwani hata Mei 6, timu hiyo ikilala 5-0, kocha alikuwa huyo huyo. Kabla ya hapo, kocha mzalendo wa mwisho Yanga kuiongoza timu hiyo dhidi ya Simba alikuwa Kenny Mwaisabula mwaka 2004.
7.Hadi sasa, Juma Kaseja ndiye mchezaji wa Simba aliyecheza mara nyingi zaidi dhidi ya Yanga, mara 23, akifuatiwa na Malota Soma mara 21. Kaseja akipangwa leo, atafikisha mechi 25 za kucheza kwenye mapambano ya watani wa jadi, tangu mwaka 2003 ikiwemo na ile ya Aprili 19, 2009 aliyoidakia Yanga dhidi ya Simba SC, mechi yake ya kwanza ikiwa ni ya Aprili 20, mwaka 2003 akikaribishwa na kipigo cha mabao 3-0, yaliyotupiwa nyavuni na Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
8.Kenneth Pius Mkapa anabakiwa kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi za Simba na Yanga, 33 akifuatiwa na Edibily Lunyamila pia wa Yanga aliyecheza mechi 26, Kaseja 24, Malota Soma 21.
9.Hili linakuwa pambano la 12, kwa watani wa jadi kukutana Uwanja mpya wa Taifa tangu ufunguliwe, awali katika mapambano 11 yaliyopita, Yanga ilishinda mechi tano, Oktoba 26, 2008 (1-0), Oktoba 29, 2011 (1-0), Julai 10, 2011 (1-0), Desemba 25, 2009 (2-1) na Agosti 18, 2010, iliposhinda kwa penalti 3-1 baadaya ya sare 0-0, wakati Simba imeshinda mechi nne, Oktoba 31, 2009 (1-0), Aprili 18, 2010 (4-3), Agosti 17, 2011 (2-0) na Mei 6, 2012 (5-0), wakati timu hizo zimetoka sare mara mbili Uwanja huo, Aprili 19, 2009 (2-2) na Machi 5, 2011 (1-1).

Habari na picha kwa hisani ya Bin Zubery Blog

No comments: