ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 22, 2012

Kijana afungwa miaka 30 kwa kumbaka mzee

Morogoro
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani hapa imemhukumu Shaabani Idd (36) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka bibi wa miaka 80 (jina limehifadhiwa) na kumsababishia maumivu makali.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ambao haukuwa na shaka yoyote katika kuthibitisha shtaka hilo.
Akisoma hukumu hiyo hakimu Isaya alisema kuwa hukumu hiyo itakuwa fundisho kwa mshtakiwa na wanaume wengine ambao wamekuwa wakiwabaka ajuza kutokana na tamaa za kimapenzi na wengine kwa imani za kishirikina jambo ambalo alisema ni kosa kisheria.
Akijitetea ili mahakama impe adhabu ya huruma mshtakiwa huyo alidai kuwa anafamilia inayomtegemea na kwamba ni mkosaji wa mara ya kwanza hata hivyo mahakama ilitupilia mbali utetezi huo baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo.
Upande huo wa mashtaka ulidai kuwa vitendo vya ubakaji mkoani hapa vimekuwa vikiongezeka kwa kasi wakati wanaofanyiwa hivyo kwa kiasi kikubwa ni ajuza na watoto wadogo hivyo adhabu kali ndio suluhisho la vitendo hivyo.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo hakimu Isaya alisema kuwa amezingatia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili na kwamba mshtakiwa anayo haki ya kukata rufaa mbele ya Mahakama Kuu endapo atakuwa hakuridhishwa na hukumu iliyotolewa mahakamani hapo.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Simon Feo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, Februari 2 mwaka huu saa 11 jioni kwenye Mto Ngerengere uliopo Tungi Manispaa ya Morogoro.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati ajuza huyo alipokuwa akichota maji kwa ajili ya kuoga, hata hivyo mshtakiwa huyo aliposomewa shtaka hilo kwa mara ya kwanza alikana na hivyo upande wa mashtaka kulazimika kupeleka mashahidi mahakamani hapo ili kuthibitisha shitaka hilo.

No comments: