ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 22, 2012

Uamsho wapewa nafuu ya dhamana


Viongozi saba wa Jumuiya ya Uamsho wamepunguziwa masharti ya dhamana na Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe, huku watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakishindwa kujitokeza kuwadhamini tangu dhamana ilipowekwa wazi na Mahakama Novemba 4 mwaka huu.
Hatua ya kupunguziwa masharti ya dhamana, imekuja baada ya wakili wa upande wa utetezi, Salum Tawfq na Abdallah Juma kuomba masharti yaangaliwe upya kufuatia uwezo mdogo wa washitakiwa na watumishi wa umma kuogopa kujitokeza kuwadhamini.
Alidai tangu dhamana hiyo kuwekwa wazi, wateja wao wameshindwa kuyatekeleza kutokana na kipato cha Wazanzibari kuwa kidogo, na washitakiwa kushindwa kumudu kuweka dhamana ya Shilingi milioni moja kwa kila mshitakiwa na wadhamini wawili kwa kiwango kama hicho.
Alidai sharti la kila mshitakiwa kuwa na wadhamini watatu ambao ni watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nalo limekuwa ni kikwazo kwa wateja wao kutokana na kesi yenyewe kuihusu Serikali dhidi ya Uamsho.
Alidai kwamba pamoja na Mahakama hiyo kutaka uongozi wa chuo cha mafunzo, kuwapatia washitakiwa hao huduma zote muhimu kama ambazo wanapatiwa mahabusu wengine, amri hiyo ya mahakama bado haijatekelezwa, zaidi ya kupewa haki ya kubadilisha nguo na kutonyolewa tena ndevu kama awali.
"Tunashukuru angalau wamepewa fursa ya kubadilisha nguo na hawajanyolewa tena ndevu, lakini bado wananyimwa fursa za kukutana na ndugu na jamaa zao, fursa ya kusoma Qur'an tukufu na kushiriki ibada ya pamoja ya sala ya Ijumaa, pamoja na kufungiwa kila mmoja katika selo yake kwa muda wa saa 24 tangu walipowekwa kizuizini," alidai Wakili huyo.
Alieleza kuwa vitendo hivyo vinakwenda kinyume na sheria namba 7 kifungu cha 41 cha mwenendo wa makosa ya jinai, juu ya haki ya washitakiwa kuwasiliana na mawakili wao na kupata huduma za hospitali na mambo mengine wanapokuwa chini ya ulinzi au uangalizi maalum.
Upande wa mwendesha mashitaka wa Serikali, ukiongozwa na Ramadhan Abdallah na Amour Ame, ulidai hawana pingamizi na washitakiwa kupunguziwa masharti ya dhamana kwa vile ni jukumu la Mahakama lakini kama wahusika haki zao za kikatiba zimevunjwa, wana haki ya kufungua kesi ya madai katika mahakama kuu.
Ramdhan alieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 25 A (1), ya katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984 imetoa uhuru kwa mtu yeyote kufungua shauri katika mahakama kuu iwapo ataona kuwa katiba imevunjwa au inavunjwa au inaelekea kuvunjwa.
Hakimu Msaraka Ame Pinja alieleza kukubaliana na hoja ya kupunguza masharti ya dhamana na kutaka kila mshitakiwa kuweka dhamana ya fedha taslimu Sh. 500,000 na wadhamini wawili kwa kiwango kama hicho, kuwasilisha hati ya kusafiria au kitambulisho cha Mzanzibari mkazi na wadhaminiwe na watumishi wawili badala ya watatu ambao lazima wawe ni wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi waliofikishwa Mahakamani hapo ni pamoja na Amir Farid Hadi Ahmed, Sheikh Mselem Ali Mselem, Sheikh Azzan Khalid Hamdan, Sheikh Mussa Juma Issa, Sheikh Suleiman Juma Suleiman, Sheikh Khamis Ali Suleiman na Sheikh Hassan Bakari Suleiman na kama ilivyo ada walifikishwa chini ya ulinzi mkali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: