Advertisements

Monday, December 31, 2012

MAISHA NDIVYO YALIVYO: Fundi nguo amenizimia nilipotaka anishonee nguo zangu, nifanyeje?


NA FLORA WINGIA
Heri ya Mwaka Mpya msomaji wangu. Naamini kesho utaumaliza mwaka salama na panapo majaaliwa ya Mola wetu tuonane tena mwaka 2013. Wakati tunafunga na kuukaribisha mwaka mpya, nikuache na kituko hiki kilichotokea mwaka huu unaoisha 2012.

Naam. Suala la mahusiano bado limegubikwa na mitego mingi. Lakini mitego hii inategemea jinsi mtu ataitegua salama pasipo madhara. Na hiyo ndiyo changamoto kubwa iliyofichika ambayo wengi wetu hawaijui. Hebu sikia mifano ifuatayo, kisha nawe msomaji utoe maoni yake tuelimishane.

Yupo msomaji mzuri wa safu hii amenitumia ujumbe ufuatao kupitia simu inayopatikana mwishoni mwa makala haya. Anaanza hivi;-

“Nimempata mchumba (binti) ambaye tulikuwa tunawasiliana huku tukiwa hatufahamiani. Kilichotokea ni kwamba niliyekuwa nampigia simu nilikosea namba hivyo ikaenda kwa mtu mwingine.
Nilipogundua siye niliyekuwa nampigia, nikakata simu. Lakini baadaye yule niliyekosea namba yake nikajikuta nampigia tena simu na kumuomba tuwe marafiki.

Hatimaye urafiki ulizidi nikajikuta nampenda nikaamua kumwambia tuwe marafiki naye akaniambia hawezi kusema ndiyo wakati hatufahamiani.

Ndipo nilipokutana naye uso kwa uso tukakubaliana mpaka leo tumejikuta ni wachumba. Nampenda sana namshukuru Mungu pia kwa sababu ameokoka kama mimi na wote kwa furaha tunamjua Mungu. Namuomba Mungu amjalie asije nisaliti siku moja. Nampenda sana.

Ndiyo hivyo ila nina mashaka maana bado nawaza hivi inawezekana kweli au ni ndoto au ana mtu wake ananidanganya, but all in all nampenda.(naomba namba yangu ya simu na jina visiandikwe gazetini).

Naam. Mpenzi msomaji huyo ni kijana aliyejaribu bahati yake na sasa amempata mchumba. Changamoto yake kubwa ni namna ya kumlinda mchumba huyu asimponyoke.

Bado anayo mashaka kwa kuwa haamini njia aliyopitia ingeweza kumpatia mwenza wake kirahisi namna hiyo.

Lakini yote ni mipango ya Mungu na mke au mume mwema hutoka kwa Mungu. Maandiko matakatifu ya Mungu yanasema hivyo. Naamini Mungu huyu tunayemtegemea ndiye atakayewabariki na hatimaye waweza kufunga ndoa takatifu iliyojaa baraka tele.

Wakati kijana huyu akitafakari uchumba wake, hebu msikie msomaji mwingine binti ambaye naye amejikuta katika kishawishi kikubwa cha mahusiano ambayo haelewi mwisho wake utakuwa ni nini.

Ametuma ujumbe mfupi wa simu unaosomeka namna hii;-

“Shikamoo, mimi kuna fundi mmoja nilimpelekea nguo zangu, basi akaomba namba yangu ya simu. Lakini nilivyomuona ananipenda sababu ananirushia hela, ananipa hela.

Chaajabu pia ananipigia kila siku lakini bado hajaniambia kitu ila naona anashindwa kuongea sababu mimi na yeye nilimjua baada ya kupeleka nguo zangu. Naomba nishauri.”

Mpenzi msomaji, huyu ni binti ambaye amejikuta anarubuniwa na fundi nguo aliyempelekea nguo amshonee. Si unajua tena mafundi nguo anapompima mwanamke anamgeuza geuza ili kupata vipimo sahihi.

Lakini wengine vijimate huwajaa midomoni kutamani maumbo ya wateja wao. Wapo wenye mishepu utadhani walipendelewa zaidi ya wengine. Na siyo ajabu fundi yule alivutiwa na umbo la bibie, hivyo akavunja mwiko wa kazi na kulazimisha mahusiano.

Tazama giya yake ya kumrushia binti vijihela kwenye simu ili amvute karibu. Binti huyu katika ushauri wangu nilimwambia asikubaliane na kishawishi hicho. Huyo jamaa ni mharibifu na inawezekana hiyo ndiyo tabia yake kwani hupata wateja wengi wa kila aina.

Kwanini amrushie hela wakati hawajakubaliana chochote? Huyo ni mharibifu na ndiyo maana anatumia nguvu ya vijihela vyake ili kumshawishi bibie.

Nikamwambia amweleze bayana kwamba aache kutuma vihela vyake hivyo na ikiwezekana avijumlishe atafute shahidi na kwenda kumkabidhi kisha aache mawasiliano naye. Je, nawe msomaji wangu, unampa ushauri gani? Tuma kupitia simu iliyoko mwishoni mwa makala haya.

Mahusiano yamegubikwa na mitego mingi sana.Wapo wanaotafuta mahusiano kwa kutumia fedha, wengine wanatoa huduma mbalimbali kama vile kugharimia ada, kumnunulia mtu simu, gauni, shati na vijizawadi mbalimbali vya kumvutia mtu ili akubali kuingia kwenye mahusiano.

Naishia hapa ili nawe uchangie na ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

1 comment:

Anonymous said...

dj luke ndo wewe waliokutumia ujumbe huu au sijaelewa kidogo hi topi nifafanuliya nani katumiwa ujumbe na kuweka hapa hadhari ili tujifunze?

mimi naona ulicho mshauri ni poa kabisa ni kweli kwa nini mtu atumiye nguvu ya pesa kutaka penzi lakin kwa upande mwinginewe ni poa tu dunia ya leo pesa kama huna au huwezi kuzitumia basi huwezi kusonga mbele hatea ukimpata mlokole wako kuna situ utataka kumtoa out mkavinjari na maisha japo ka dinner au lunch je kama huna pesa utafanyaje kuna siku atakuwa na tatizo na pesa je utafanyaje so jamaa kamuanzi na mapema binti huyu kumuonyesha pesa si tatizo japo kuwa hajaziomba. wasichana wengi wana penda jamaa waaina hii pesa nje nje jamani TUSIDANGANYANE, JAMAA ANAYE BANA BANA PESA ZAKE BINTI HAKAWII KUMUACHA AU KUMUONA HUYO MCHUMBA BAHILI NA KUPATA MACHUNGU YA MOYO NA MWISHO WA SIKU WATAACHANA TU AKITOKEA PADAJEE ATAKAYE MMWAGIA FEDHA FEDHEHAAA AKAMPA GOOD TIME HATOSITA HATA KIDOGO HATA KAMA ANAMPENDA MCHUMBA WAKE BAHILI MKONO WA BIRIKA.

NAKUTAKIA KHERI YA MWAKA MPYA MWEMA DJ LUKE PAMOJA NA FAMILY YAKO NA NDUGU NA JAMAA NA MARAFIKI NA WADU WENZANGU WOTE WA VIJIMAMBO

KWA KWELI LUKE UNAFANYA KAZI NZURI SANA KUTUELIMISHA SHUKRAN SANA NA UBARIKIWE SANA MKUU TAKE CARE. PEACCE MAN MUNGU AKUBARIKI SANA MKKUU