ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 16, 2013

Chadema sasa waanza kulipuana

Dk Willibrod Slaa

“Heche na Mbowe wamenifedhehesha kwa kauli zao na wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa Watanzania, hivyo nitapambana nao kuhakikisha haki yangu inapatikana,” alisema Shonza.

KATIKA kuonyesha hali si shwari ndani ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa chama hicho, Juliana Shonza amesema ameamua kumshtaki Mwenyekiti wake, John Heche kwa kumuita kuwa ni msaliti wa chama na kwamba anatumiwa na CCM na kuamua kumfukuza nafasi yake bila kutoa nafasi ya kusikilizwa.

Pia, amemlipua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa akidai kuwa amefanya ufisadi ndani ya chama kwa kujikopesha Sh140 milioni ambazo hajazilipa hadi sasa.
Mbali na hilo, amemshukia Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa kudai kuwa anatoa kauli za kukurupuka ambazo zinakiyumbisha chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Shonza alitoa kauli hizo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juu ya tuhuma zilizotolewa na mwenyekiti wa Bavicha na kuhusu kufukuzwa kwake ndani ya chama akiwa na wenzake Mtela Mwampamba na Habibu Mchange.

“Heche na Mbowe wamenifedhehesha kwa kauli zao na wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa Watanzania, hivyo nitapambana nao kuhakikisha haki yangu inapatikana,” alisema Shonza.

Shonza alisema kwamba yeye bado ni makamu mwenyekiti wa Bavicha na mwanachama halali wa Chadema kwa kuwa hadi anazungumza hakuwa amepewa barua ya kufukuzwa kwa kuwa kikao kilichotoa uamuzi huo ni batili.

Alisema kikao kilichoitwa ni cha kamati tendaji na kufikia maamuzi ya kumfukuza kilikuwa batili kwa kuwa katiba pamoja na mwongozo wa Bavicha ulikiukwa, kitu kinachosababisha aeleze kuwa uamuzi uliotolewa na kikao hicho yalikwishapangwa na viongozi wa kitaifa.

“Nasisitiza kwamba ni ukweli uliowazi kwamba ajenda na maazimio ya kikao hicho yalikwishaamuliwa hata kabla ya kikao hicho, kwa sababu taarifa za kufukuzwa kwetu zilikwishaanza kusikika kwenye mitandao ya kijamii kabla hata ya kamati tendaji batili,”alisema Shonza.

Alisema mkakati wa Heche na vibaraka wake umejikita kutukuza ukanda ndani ya chama waziwazi, akieleza kuwa watu waliofukuzwa ndani ya chama hicho wanatokea Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini haswa Mbeya wakati vijana wa Kaskazini wameachwa kwa madai kuwa wametoa ushirikiano.

“Natarajia kuomba ufafanuzi wa kikatiba juu ya shutuma zilizotolewa dhidi yangu na Heche kwa kuwaaminisha Watanzania uongo wake,”alisema Shonza.

Kuhusu Mbowe
Alisema kuwa amesikitishwa na kauli ya kiongozi wake huyo katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba, madai aliyoyatoa ni ya kitoto kwani ni kitu cha kushangaza kwa kuwa yeye Juliana hayajui ni madai gani hayo.

Alisema kama madai ambayo Mbowe anadai ni ya kitoto ni ya yeye kuhoji kwa nini chama hakiweki akiba kwenye akaunti kwa ajili ya uchaguzi wa 2015 kama ilivyokubaliwa kwenye baraza kuu basi itakuwa ni ajabu.

Kuhusu Dk Slaa
Alisema inashangaza kwa mwenyekiti wa chama anafumbia macho hatua ya Dk Slaa kujikopesha pesa ya ruzuku ya Watanzania zaidi ya Sh140 milioni, kwani ni kinyume na utaratibu uliopo.

Shonza alisema Dk Slaa kama katibu mkuu wa chama ndiye mtendaji, hivyo fedha hizo hakukopeshwa bali amejikopesha mwenyewe kwa masilahi yake binafsi. Katika hali isiyokuwa ya kawaida aliibuka kijana mmoja katika mkutano huo jana akidai kuwa ametumwa kuwasilisha barua za kufukuzwa kwa Shonza kwenye chama lakini hazikupokewa na wahusika.

Akizungumzia suala hilo, Heche alisema uamuzi ulishafanywa na kamati tendaji ya baraza na kwama vielelezo vya kwamba Juliana ni msaliti vipo na hali ya usaliti itamwandama milele.
“Rufaa ya Chadema haikatwi kwenye vyombo vya habari, angekuwa na nidhamu angeenda kukata rufaa kwenye vikao vingine vya chama,”alisema Heche.
Alipopigiwa Dk Slaa ili kujibu tuhuma zilizotolewa na Shonza, simu yake ilipokelewa na mtu ambaye hakujitambulisha akieleza kuwa Dk Slaa yuko kwe mkutano wa hadhara.
“Dk yuko kwenye mkutano,”alisema.

Kwa upande wake, Mbowe hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani

Januari 9 mwaka huu, Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa na gazeti hili akieleza kuwa wao hawahusiki na hujuma yoyote ndani ya Chadema, hivyo chama hicho kitafute mchawi wake chenyewe.

Nape alisema
CCM haihusiki na mgogoro wowote ndani ya Chadema hivyo kijipange na kutafuta mchwi wake.

Mwananchi

No comments: