Tuesday, March 12, 2013

Aibu,vyoo vya shule karne ya 21

Huduma za vyoo katika shule mbalimbali nchini inaonekana mbaya kiasi cha kutishia uhai wa wanafunzi na walimu wanaovitumia.
Wataalamu wa masuala ya elimu na saikolojia, wanaibainisha pia kuwa vyoo vinapokuwa duni, vinachangia kudumaza maendeleo sekta ya elimu kwa sababu wanafunzi wenye kuhara, kwa mfano au wa kike hulazimika kutokwenda shule hasa wanapokuwa hedhi kwa vile wanashindwa kujisitiri.
Shule ina wanafunzi 400 haina vyoo
Shule ya Msingi Lugalo iliyopo Kata ya Mazombe, wilayani Kilolo mkoani Iringa yenye zaidi ya wanafunzi 400 ni kati ya shule ambazo kwa miezi mitatu hivi mfululizo  imekuwa ikielezwa kutokuwa na vyoo thabiti, achilia mbali uhaba mkubwa wa madawati, kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Kinyanya.
Shule ina matundu 16 ya vyoo vilivyojengwa kwa miti, ambayo imeoza, mwalimu huyo mkuu ana hofu huenda ikafungwa kwa kuonekana kama eneo lisilo salama kwa watoto, kwani wanaweza kupoteza maisha kwa kutumbukia chooni. Kati ya shule 96 za msingi za wilaya hiyo, Lugalo mara kadhaa imekuwa ikishika nafasi ya tano, hata hivyo Mwalimu Kinyanya, ana hofu huenda maendeleo haya yakawa mabaya ikiwa mazingira hayataboreshwa haraka.
Watafiti wabainisha
Ripoti iliyotolewa mapema mwezi huu na Shirika la Water Aid, lenye ofisi nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, inaonyesha kuwa hali ya vyoo katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, inasikitisha, huku watoto wa kike wakielezwa kuathirika zaidi kutokana na maumbile yao kuhitaji zaidi usafi hasa wanapokuwa hedhi.
Mkataba wa Dakar wa elimu kwa wote, unataka ifikapo mwaka 2015 watoto wote wawe wana uwezo wa kupata elimu ya msingi iliyo bora ikiwamo kuwa na uhakika wa huduma za vyoo na mazingira ya shule kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa hali inavyoonekana ni ndoto au huenda ikachukua kazi ngumu mno kwa Tanzania kutimiza hilo, kutokana na kubainika kuwa na shule nyingi kutokuwa na vyoo thabiti, zikiwamo za mijini, achilia mbali za vijijini.
Hali mbaya ya vyoo shuleni
Ripoti hiyo inasema,  Shule ya Msingi Mpalanga iliyopo Chamwino mkoani Dodoma ina wanafunzi 1,022 huku ikiwa na matundu 10 tu ya vyoo, hivyo kusababisha wanafunzi kwenda chooni kwa foleni.
Choo cha matawi ya majani Shule ya Zejele
Hali kadhalika shule ya Zejele iliyopo Chamwino, mkoani Dodoma nayo vyoo vyake licha ya kujengwa kwa miti, imeezekwa kwa majani na udongo, huku milango ikiwa wazi, na baadhi ya vyoo vikiwa vinatumia milango ya matambala yaliyochakaa.
Jambo hili limekuwa likisababisha baadhi ya wanafunzi kujisaidia porini ambako angalau mtu anaweza asionekane anapojisaidia kuliko chooni.
Ili kuangalia kama vyoo vinasaidia kuimarisha ari ya watoto kusoma au la, WaterAid ilijenga vyoo vyenye matundu 20 hivi karibuni katika shule hiyo na katika utafiti walibaini kuwa kuwapo kwa vyoo vizuri vinachangia ongezeko la mahudhurio ya watoto shuleni.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Salvina Maswaga (12) anasema “Vyoo tulivyokuwanavyo mwanzo vilikuwa vibaya sana, kulikuwa hakuna milango, vilikuwa vidogo na vichafu, hivi vya sasa vinakufanya hata utamani kuja shuleni.”
Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo aliyetajwa kwenye ripoti hiyo kwa jina la Mama Rugakingira, anasema, “Kwa mwezi wasichana hukosa shule kati ya siku mbili au tano kutokana na mazingira ya shule, hasa kama wanakuwa hawana uhakika wa kujisitiri wanapokuwa kwenye ‘siku zao’, suala hili linachangia kuporomoka kwa maendeleo yao shuleni.”
Anasema mtoto wa kike anapokuwa katika hali hiyo anahitaji sehemu ambayo ni safi, yenye kumfanya asionekane kwa urahisi na mtu hasa anapobadili mavazi yake kwa lengo la kujihifadhi.
Athari za kiafya kwa choo duni
Mtaalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Amana, Jijini Dar es Salaa, Dk Samweli Chita, anasema kwa kiasi kikubwa vyoo visivyofaa vina athari kubwa kwa watoto wa kike, kwani kwa namna walivyo wanahitaji usafi wa hali ya juu hasa wakiwa katika hedhi.
“Msichana anapokuwa kwenye hali hiyo anatakiwa kubadilisha vazi lake la kujihifadhi aidha kama ni tambala au pedi, angalau mara tatu mpaka nne kwa siku, ingawa kiwango cha kawaida ni mara tatu, anatakiwa abadilishie kwenye mazingira  mazuri, yenye usafi au la anaweza kupata wadudu wanaoweza kuathiri afya yake,” anasema na kuongeza:
“Wakati akibadilisha inatakiwa choo kiwe kinampa nafasi ya kuinama na kuitoa, kujisafisha na kuitupa isionekane kwa sababu mtu mwingine akija kuiona hasa wa kiume kunaweza kumwathiri mtoto yule kisaikolojia.”
Anasema pia kuwa, mbali na magonjwa ya milipuko na kuhara, vyoo vichafu na visivyo na maji ni rahisi kuwaambukiza watoto wa kike magonjwa UTI yaani Urinary Tract Infection; ugonjwa unaoambatana na mfumo mzima wa njia ya mkojo.
Kisaikolojia ina athari gani?
Mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga, anasema, “Inamfanya mtoto kulala akiwa amechoka, kwani anaongezewa mzigo wa kuwaza zaidi na ilivyo kawaida hasa anapoumwa hedhi au kwa watoto wa kiume kama ana tatizo la kuhara.Kwa ujumla ni tatizo linalochangia kuharibu uwezo wa kufikiri wa mtoto, ndio sababu huwa tunashauri watoto kusomea mazingira mazuri, kwani yanawashawishi kusoma vizuri, hiyo inasaidia kukuza maendeleo yao na taifa kwa ujumla.”
"Kujenga mfumo wa elimu unaofanya kazi vizuri kunahitaji zaidi ya kuwa na matundu ya vyoo. Nchi inapaswa kuwa na madarasa ya kutosha, walimu na vifaa vya shule kwa ajili ya kutosheleza watoto wote, kutaharakisha maendeleo katika sekta hii,” anasema.
Serikali ya Tanzania ilitenga  Sh721 bilioni katika bajeti yake ya 2012/2013, fedha ambazo nyingi zinakwenda kuwalipa walimu na watu wengine katika sekta ya elimu pamoja na huduma nyingine  zilizo nje ya kuimarisha mazingira ya shule kama ujenzi wa vyoo, huku ikiacha maswali ya nini hatima ya sekta hiyo muhimu ikiwa hali ndiyo hii.
Mwananchi

No comments: