Tuesday, March 12, 2013

Madeni Simba yamponza Liewig

kocha Mfaransa Patrick
Liewig wa timu ya Simba.
Hali ya kifedha ndani ya klabu ya Simba imeanza kuibua hofu baada ya kudaiwa kuwa kocha wao Mfaransa Patrick Liewig hajalipwa mishahara yake ya miezi miwili huku pia akinyang'anywa gari alilokuwa akitumia kutokana na uongozi wa klabu hiyo kutolipa madeni ya huduma walizopata katika hoteli mbili jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilidai jana kuwa kocha Liewig amenyang'anywa gari alilokuwa akitumia aina ya Toyota GX110. ambalo limeshikiliwa na hoteli moja ya Kariakoo jijini Dar es Salaam inayodai Sh. milioni 28.
Imedaiwa kuwa baada ya kulimbikiza deni katika hoteli hiyo ya awali, uongozi wa Simba ukahamia katika hoteli nyingine iliyopo pia katika eneo la Kariakoo na kulimbikiza deni jingine linalozidi Sh. milioni 20 na mwishowe, wakafukuzwa juzi baada ya uongozi wa hoteli kuhofia kuwa watapata usumbufu katika kulipwa fedha zao.
Imeelezwa zaidi kuwa mbali na kushikiliwa kwa gari alilokuwa akitumia Liewig, pia basi dogo la klabu hiyo linashikiliwa kwa sababu ya madeni.

Uongozi wa Simba ulikiri kuzuiwa kwa timu yao kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union juzi kutokana na kudaiwa na uongozi wa hoteli, lakini umekanusha kuwapo kwa taarifa nyingine kuwa kuna hujuma kutoka kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kwamba klabu hiyo inadaiwa jumla ya Sh. milioni 51 na hoteli mbili za Kariakoo jijini Dar es Salaam; moja ikidai Sh. milioni 25 na nyingine Sh. milioni 26.

Alisema madeni hayo yametokana na huduma walizokuwa wakipata kwa muda mrefu za malazi na chakula kwa wachezaji na makocha wao.

Mtawala alisema kwamba walishangazwa na tukio la kuzuiwa kwa timu yao wakati hadi kufikia saa 6:00 mchana walikuwa na mmiliki wa hoteli husika ambaye hakuonyesha kuwapo na nia hiyo aliyodai kuwa imeidhalilisha timu yao.

"Sisi tunafanya nao biashara tangu msimu huu wa ligi ulipoanza ambapo timu ikiwa na mechi Dar es Salaam na kila mechi inapochezwa siku inayofuata tunamlipa kati ya Sh. milioni 8 na Sh.milioni 15... ila kwa hili ametudhalilisha kwa sababu alipaswa atupe notisi," alisema Mtawala.

Katibu huyo aliongeza kuwa yote hayo yanatokana na timu yao kufanya vibaya na hivyo kupata mapato kidogo ya milangoni, akitolea mfano mechi dhidi ya Coastal waliyoambulia Sh. milioni 8 tu ambazo hazitoshi kulipia madeni yanayowakabili.

"Tuko kwenye mazungumzo na wadau wetu pamoja na mama Rahma...tunaweza kuwalipa jioni hii (jana jioni) au kesho (leo) asubuhi," alisema Mtawala.

Aliongeza kuwa hata hivyo, Simba pia inazidai taasisi kadhaa na hivyo wanawaomba wanaowadai kuwa na subira kwani watawalipa tu.

Mtawala aliongeza kwamba kufuatia hali hiyo uongozi uko katika hatua ya mwisho ya kuwalipia pango ya nyumba makocha wake pamoja na wachezaji wa kigeni.

Mmiliki wa hoteli mojawapo inayoidai Simba, Abdul Fattah, alisema kwamba hivi sasa hawataki klabu hiyo iendelee kulimbikiza deni kwa sababu hakuna urafiki katika biashara.

Hivi karibuni, Simba imejikuta katika wakati mgumu kutokana na matokeo yasiyoridhisha na kuwalazimu baadhi ya viongozi wake kujiuzulu, wakiwamo makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Gofrey Nyange 'Kaburu' na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hanspope.
CHANZO: NIPASHE

No comments: