ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 18, 2013

Profesa Mbwete abaini kuwapo mtambo wa kughushi vyeti




Makamu Mkuu wa  Chuo Kikuu Huria  (OUT),  Profesa Tolly  Mbwete, amesema  OUT imebaini kuwapo mtambo unaotumika kughushi vyeti.

Alisema  hayo yalibainika  hivi karibuni baada ya mmoja wa waajiri  kupata  hofu wakati wa kuwafanyia usaili watumishi wapya alipokuwa anachunguza vyeti vyake.

Alitoa taarifa hizo  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na programu maalum ya kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama)  kwa walemavu.

Alikuwa akizungumza mjini Dodoma ambapo Chuo hicho, Mamlaka ya Elimu Nchini (TEA), Shirika la Sightsavers  na Chuo cha Ualimu cha Patandi wanaendesha maonyesho ya program hiyo.


Bila kufafanua zaidi,  alisema  mtambo huo ulibainika baada ya mmoja wa waajiri kupata hofu kuhusu uhalali wa cheti cha mmoja wa watu waliokuwa wameomba kazi na kutoa taarifa.

“Tunatoa  taarifa kwa wananchi  wasitafute  njia rahisi ya  kupata sifa za elimu wajiunge na chuo hiki wasome maana tutawagundua baada ya dakika mbili tukikipata cheti hicho,”alisema.

Alisema baada ya uchunguzi wa cheti hicho walibaini kuwapo kwa asilimia 30 ya uhakika wa vitu vilivyopo ndani ya cheti  halisi  vinavyotolewa na chuo chake.

Suala hilo limepelekwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumzia kuhusiana na programu hiyo ya Tehama, Kaimu Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Ukuzaji wa Raslimali wa TEA, Slyvia Gunze, alisema wanaohusika na programu hiyo ni wenye ulemavu wa kutoona, uoni hafifu na wasiosikia.

Alisema majaribio ya awali ya mpango  huo yamewezesha wanafunzi hao kujifunza kuwa  walimu wa walimu wengine na pia kuongeza uwezo wa kufundisha kundi hilo katika vyuo hivyo.

“Tunahitaji kuwafundisha watu wengi sana ili waweze kunufaika na teknolojia hii ambayo imeonekana kuwa na manufaa kwa kundi hili,”alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Sightsavers, Janeth Bushiri, alisema  mradi wa majaribio ulianza mwaka juzi  ambapo watu 15 walinufaika na mafunzo hayo ya siku 15.

“Hii ilikuwa kama chachu ya kuhamasisha watu wengi zaidi  kunufaika na mafu
nzo hayo  na mwaka jana  watu 27 kutoka Tanzania Bara na Visiwani walinufaika na mafunzo haya,”alisema.

Akizungumzia kuhusiana na programu hiyo, Profesa Mbwete alisema programu hiyo imewezesha kuongeza uwezo wa kutoa elimu kwa watu wenye mahitaji Muhimu.

“Kama mnavyojua elimu ya OUT inategemea sana mwanafunzi  kutumia mitandao mbalimbali ni muhimu kwa kundi hili kujifunza Tehama ili waweze kuitumia teknolojia hii,”alisema.
        
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: