ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 14, 2014

AFUNGWA JELA MIAKA 15 KWA KUMUAMBUKIZA MWANAMKE VIRUSI VYA UKIMWI KWA MAKUSUDI

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEipY6q5QSgFjrSwlvYDAbI-IliziXWRp0Lw6SRbJtSg9LCEs86HicHBzpXcVLMgBLQ21CJuAAGbLFlHzivo05qBcyN1npSfEm1oPqcFigEkGC3_wMtAnWxT8weib8TfPdFfmbfuRvM3ssvg/s640/red-ribbon-hi.pngMWANAMUME mwenye umri wa makamo, Jumatatu alisukumwa jela kwa miaka 15, kwa kumwambukiza mwanamke Ukimwi maksudi wakifanya mapenzi.
Hakimu Mkazi wa Iten, Bi Rose Ndombi, alimpa Gilbert Kiptoo Barbos adhabu hiyo baada ya kumpata na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamke huyo akijua kwamba alikuwa na ukimwi.
Barbos alipatikana na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamke huyo mnamo Septemba 2, 2013, katika lojingi moja mjini Iten Kenya, akijua wazi kwamba alikuwa na virusi vya ukimwi.
Mahakama iliambiwa kwamba alifanya makosa hayo maksudi kwa kukosa kutumia kinga wakati wa kitendo hicho akijua kwamba hatua hiyo, ingemfanya mwanamke huyo aambukizwe ukimwi.
Mbali na kosa hilo, Barbos alikabiliwa na mashtaka mengine  mawili ya ubakaji na wizi. Mahakama iliambiwa kwamba aliiba simu aina ya Techno ya mwanamke huyo yenye thamani ya Sh3000 na Sh1000 pesa taslimu.
Mwendesha mashtaka,  Bw Tom Chitira aliambia mahakama kwamba Barbos, na mshukiwa mwingine ambaye hakuwa mahakamani, walimwambia mlalamishi kwamba wangemsaidia kupata kazi mjini Iten. Walipofika mjini Iten, Barbos alimpeleka mwanamke huyo katika lojing’i ambako wangelala kabla ya kumpeleka kwa mtu ambaye alidai angemwajiri.
Mlalamishi aliambia mahakama kwamba Barbos alimhandaa kwamba wangelala vyumba tofauti.
“Nafikiri alinilewesha kabla ya kunipeleka katika lojing’i kwa sababu nakumbuka nikikataa pendekezo lake la kulala chumba kimoja na mtu mgeni kwangu kabla ya kujipata katika chumba alichokuwa siku iliyofuata,” mwanamke huyo aliambia mahakama. Alisema alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Iten na mshtakiwa akasakwa na kukamatwa.
Maafisa wa polisi walimshauri mwanamke huyo aende kupimwa baada ya kupata dawa za kuzima makali ya ukimwi (ARVs) walipomkamata Barbos.
Ripoti ya daktari iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha kwamba baada ya kupimwa, iligunduliwa mlalamishi alikuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi.
Ubakaji
Hata hivyo, Bi Ndombi  hakumpata Barbos na hatia ya ubakaji akisema upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo kulingana na viwango vinavyohitajika kisheria, lakini akampata na hatia ya kuambukiza mwanamke huyo ukimwi na kumuibia.
Akimhukumu, Bi Ndombi alisema Barbos atafungwa jela miaka 15 ili kuwa funzo kwa wengine wanaofanya makosa kama hayo. Alisema kwamba sheria iko wazi kwa wanaoambukiza wengine ukimwi maksudi.
Alimhukumu mshtakiwa kufungwa jela miezi sita kwa kosa la wizi na akaagiza kila hukumu itekelezwe baada ya nyingine. Alimpatia mshtakiwa siku 14 za kukata rufaa asiporidhika na hukumu hiyo.

No comments: