ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 14, 2014

POLISI TABORA WAKANUSHA KUMUUA MKUYA


Polisi mkoani Tabora imekanusha kuhusika  na mauaji ya Mbeyu Mkuya (35), kama inavyodaiwa  na ndugu wa marehemu huyo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo habari mjini hapa na Kamanda wa  Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda ilisema uchunguzi wa polisi, umebaini kuwa madai yaliyotolewa na ndugu wa marehemu, hayana ukweli wowote;  kwani marehemu alikuwa na ugomvi na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi wenzake.

 Taarifa hiyo ilifafanua kwamba uchunguzi wa awali wa polisi, ulibaini kuwa  siku ya tukio kuna watu wasiojulikana, walienda nyumbani kwa mpenzi wa marehemu (jina limehifadhiwa) katika  mtaa wa Kanoni Kata ya Isevya  na kumteka kisha kumpeleka kusikojulikana mtu huyo.

Walifanya hivyo kwa madai  kwamba alikuwa kawadhulumu fedha wenzake, walizokuwa wameiba katika matukio mbalimbali ya uhalifu. 

Kaganda  alisema kuwa uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa, marehemu huyo alikuwa akijihusisha na vitendo mbali mbali vya kihalifu, ukiwemo ujambazi wa kutumia silaha za kivita.

 Alisema taarifa za kiintelijensia zinaeleza kwamba Mkuya aliwahi kufanya matukio ya uhalifu ya wizi wa kutumia silaha mkoani Mwanza maeneo ya Nyegezi  Kona na alifunguliwa jalada la kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha eneo la kijiweni Nyegezi Mwanza, akishirikiana na watu wengine watatu ambao bado wanasakwa na polisi.

 Taarifa hiyo ilisema Mkuya aliwahi kufikishwa mahakamani kwa kesi ya jinai 214/2010, akikabiliwa na mashitaka ya unyang'anyi wa kutumia silaha mkoani Mwanza.

Kamanda huyo alivitaka vyombo vya habari, kuwa makini na watu wanaowafuata kutoa taarifa zao, kwamba wawe makini na watu wa namna hiyo kwani wanaweza kuleta mgongano kati ya jamii, wanahabari na jeshi la polisi.

Hivi karibuni ilidaiwa kuwa Polisi walihusika katika kumuua Mbeyu Mkuya kwa kumpiga risasi mgongoni. Mwili wake uliokotwa na wananchi katika pori la Ibiri wilaya ya Uyui. Tukio hilo lilitokea Aprili 7, mwaka huu

No comments: