Kikosi cha timu ya Kagera Sugar.
Na Sweetbert Lukonge
KAGERA Sugar inatarajiwa kukipiga na Simba, kesho Jumamosi kisha itakutana na Yanga, Jumatano ijayo, lakini benchi la ufundi la timu hiyo ya mkoani Kagera limesema ‘litakaza’ kwenye mechi zote hizo.
Ikiwa Kagera itaizuia Yanga kupata ushindi, maana yake ni kuwa, Azam FC itakuwa imetwaa ubingwa kwani mpaka sasa inahitaji pointi sita katika mechi tatu zilizosalia.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Mrage Kabange, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanazifunga Simba na Yanga lakini zaidi akasisitiza nia yao ni kuifunga Yanga ili hata kama Azam ikiwa bingwa, kwao ni sawa tu.
“Tunaendelea vizuri na maandalizi yetu, ambapo tutaanza na Simba hii na baada ya hapo tutatua Dar es Salaam kwa kuishikisha adabu Yanga, kwani lengo letu ni kuitandika ili na sisi tuweze kumaliza ligi kuu tukiwa katika nafasi ya juu.
“Yanga wasitegemee kabisa kuwa watatufunga, kama walifanya hivyo ilikuwa ni zamani, lakini sasa wajiandae kupokea maumivu lakini pia tunataka kufanya hivyo ili kuleta mabadiliko msimu huu kwani tumeshazichoka Simba na Yanga, tunataka wengine nao watawale soka letu,” alisema Kabange.
No comments:
Post a Comment