By Israel Saria on August 7, 2014
*Vidal akaribia Man United, Liverpool Falcao
*Juve wamtaka Wilshere, Arsenal kwa Reus
Manchester United wanadaiwa kufikia makubaliano na kiungo wa Juventus, Arturo Vidal kwamba atalipwa £182,000.
Maafikiano hayo yalifikiwa na wakala wake, Fernando Felicevich lakini inaeleweka kwamba Juventus wenyewe hawajaamua kumuuza au la, licha ya kuweka Julai 6 kuwa siku ya mwisho ya kutoa uamuzi.
Vidal mwenyewe amekuwa akiwasumbua Juve ili wamwache aondoke ajiunge na Louis van Gaal na United wanasubiri kwa hamu matokeo, wakijua kwamba akilazimisha kuondoka bei yake inaweza kuwa ndogo zaidi ya pauni milioni 42 anazothaminishwa nazo.
Inaelezwa kwamba Vidal aliyewika na Timu ya Taifa ya Chile kwenye fainali za Kombe la Dunia amekubali kukaa Old Trafford kwa miaka mitano. Hata hivyo, pamekuwa na tetesi kuwa Van Gaal alikuwa katika hatihati ya kumsajili kutokana na matatizo yake ya goti ambayo hujirudia.
Katika habari nyingine, Liverpool wamejitosa kutaka kumsajili mchezaji wa Monaco, Radamel Falcao. Wanataka pia kumsajili mshambuliaji nyota wa Milan, Mauro Icardi. Beki wao wa kati, Daniel Ager amemwomba bosi Brendan Rodgers amruhusu kuondoka. Anawaniwa na Arsenal na Barcelona.
Arsenal nao inadaiwa wanataka kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Marco Reus na mchezaji wa Manchester City, Matija Nastatic. Dili la Sami Khedira nalo limerejeshwa mezani, baada ya Real Madrid kusema watapunguza bei ili aondoke, naye mwenyewe kuwa tayari kupunguza madai ya mshahara na posho.
Arsenal wameshangazwa pia na hatua ya Juventus kutaka kumsajili kiungo wao Mwingereza, Jack Wilshere (22) ambaye Arsene Wenger anataka acheze karibu kila mechi na anatazamwa na wengi kuwa nahodha wa baadaye hapo Arsenal, hivyo si rahisi Wenger kufikiria kumuuza.
Manchester United, hata hivyo, wamejisogeza karibu zaidi kumchukua nahodha wa Arsenal, Thomas Vermaelen, baada ya kusema wapo tayari kutoa pauni milioni 15 na wala si milioni 10 alizothaminishwa nazo. Wanachuana na Barcelona kumpata Mbelgiji huyo.
Paris Saint-Germain hawana tena nia ya kumsajili Angel Di Maria wa Real Madrid, hivyo kuacha njia nyeupe kwa Manchester United ambao wamekuwa wakimsaka. United wapo tayari kumlipa raia huyo wa Argentina pauni 120,000 kwa wiki.
CREDIT:TANZANIASPORTS.
No comments:
Post a Comment