1: BENARD MEMBE
Benard Kamillius Membe ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi na ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alizaliwa tarehe 09 Novemba 1953, katika Kijiji cha Rondo-Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini.
Membe ana shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma na ana shahada ya umahiri ya Uhusiano wa Kimataifa.
Membe aliajiriwa kwenye Ofisi ya Rais na kufanya kazi kwa miaka 6 kabla hajaanza shahada ya kwanza na baadaye alirudi vyuoni kusoma na kuhitimu shahada ya umahiri, alirejeshwa tena ofisi ya Rais kabla ya kuhamishiwa wizara ya Mambo ya Nje kuwashauri mabalozi.
Membe alianza shughuli za ubunge mwaka 2000 pale alipogombea katika jimbo la Mtama, Lindi na kushinda. Mwaka 2005 alishinda tena ubunge na kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye wizara ya Nishati na Madini kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa akichukua nafasi ya Bi. Asha Rose Migiro na aliposhinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Rais Kikwete alimteua kushikilia wizara hiyohiyo ya mambo ya nje, mahali ambapo yupo hadi leo.
2. JANUARY MAKAMBA
January Yusuph Makamba ni mbunge wa jimbo la Bumbuli lililoko mkoani Tanga na ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Makamba ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, (Mzee) Yusuph Makamba na alizaliwa tarehe 28 January 1974 na ana shahada ya kwanza ya masuala ya amani (Peace Studies) na shahada ya umahiri ya sayansi ya Usuluhishi wa migogoro.
Amewahi kufanya kazi kwenye wizara ya mambo ya nje kama Ofisa wa daraja la pili na baadaye akajiunga na timu ya kampeni ya Rais Kikwete kama mtu muhimu kwenye mipango na mikakati. Kikwete alipoingia Ikulu alimteua January kuwa “Msaidizi Binafsi wa Rais Katika Mambo Maalum”.
January aligombea ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kwatiketi ya CCM na kushinda. Katika bunge la 10 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge ya Nishati na Madini na mwaka 2011 CCM ilimteua kuwa katibu wa siasa na mahusiano ya kimataifa akichukua nafasi ya Benard Membe. January alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM na tangu mwaka 2012 yeye ndiye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
3. ASHA ROSE MIGIRO
Dk. Asha Rose Migiro ni Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, alizaliwa tarehe 09 Julai 1956 katika wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma. Ana shahada tatu za chuo kikuu, shahada ya kwanza ni ya sheria (L LB), ya pili ni shahada ya umahiri ya Sheria (L LM) na ya tatu ni shahada ya uzamivu ya sheria (PhD).
Migiro amekuwa mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na baadaye amekuwa mhadhiri mwandamizi akifundisha katika kitivo cha sheria. Amewahi kuwa Mkuu wa Idara ya Sheria za Katiba na Utawala na baadaye kuwa mkuu wa Idara ya Sheria za Makosa ya Jinai (Idara zote zipo katika Kitivo cha Sheria UDSM)
Mwaka 2000 aliteuliwa kuwa mbunge na Rais Mkapa na kisha akateuliwa kuwa waziri kwenye wizara ya Wanawake, Watoto na Maendeleo ya Jamii na ameendelea kuteuliwa katika nyadhifa za ubunge huku akikabidhiwa uongozi wa wizara hata kwenye uongozi wa Kikwete ambapo aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje kabla ya kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Naibu Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa muda wa miaka mitano.
4. AMINA SALUM
Amina Salum Ali ni mtanzania mwenye asili ya Zanzibar na alizaliwa tarehe 24 Oktoba 1956. Amina ni mhitimu wa shahada ya Uchumi, pia ana stashahada ya Usimamizi wa Fedha, shahada ya umahiri (MBA) ya Usimamizi wa Biashara katika Masoko na ana stashahada ya Biashara na Masoko ya Nje.
Balozi amina amekuwa mbunge katika Bunge la Tanzania kati mwaka 1985 – 1990, amekuwa mbunge na mwakilishi kwa wakati mmoja kati ya mwaka 1990 – 2000. Kiongozi huyu pia ameshikilia nyadhifa za uwaziri katika Serikali ya Muungano na ya Zanzibar kwa miaka takribani 20 na mwaka 2006 alijivua nyadhifa za uwakilishi na uwaziri za Zainzibar ili kutumikia nafasi mpya ya uteuzi wa kuwa Mwakilishi (Balozi) wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa.
5. JOHN POMBE MAGUFULI
John Pombe Joseph Magufuli ni mbunge wajimbo la Chato lililoko mkoa wa Geita na ni waziri wa ujenzi wa Tanzania. Alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 wilayani Chato Mkoani Kagera. Kielimu, Magufuli ana Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati, ana Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati, ana shahada ya umahiri ya Sayansi na shahada ya Uzamivu ya Kemia.
Magufuli amewahi kufundisha katika Shule ya Sekondari Sengerema miaka ya themanini kisha akajiunga na mafunzo ya JKT na alipohitimu akaanza kazi katika kiwanda cha ‘Nyanza Cooperative Union (Ltd.)’ akiwa Mkemia kabla ya kuondoka hapo na kuwania ubunge.
Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995 katika jimbo la Chato na kushinda kisha akateuliwa na Rais Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu. Mwaka 2000 pia aligombea ubunge na kushinda na Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Miundombinu.
Mwaka 2005 Magufuli aligombea ubunge kwa mara ya tatu na kupita bila kupingwa, Rais Kikwete akamteua kuongoza wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na baadaye akamhamishia wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Miundombinu na baadaye ujenzi.
2 comments:
CCM hatujipendi. Really? Mtu anyeblock watu Twitter wanaomuuliza maswali ya muhimu, wanaopingana na maoni yake anafaa kua raisi wa Tanzania? Akiwa raisi atawafanyaje watu wanaopingana na maamuzi yake?
Hapo atakayeokoa jahazi letu ni Migiro na Membe.
Membe aokoe jahazi la kwenda wapi? Mtama..
Post a Comment