Wednesday, August 19, 2015

SHOGA, GARI LAKO LEO UNAOMBA LIFTI?

JAMANII mmmh! Makubwa madogo yana nafuu, hivi jamani mwenye nyumba akikamatwa anadokoa mboga si aibu eeeh? Nyama upike mwenyewe kisha udokoe? Basi wakati mwingine tuiache akili ya kawaida ifanye kazi yake na si kutumia akili za chini. Inawezekana kiburi cha barafu kushindana na jua ndicho kinatuponza.

Shoga wee! Naona mimacho imekutoka kama umeona sisimizi kameza nazi na kujiuliza leo nimekujaje kama hunielewi vile. Hebu kaa kitako nikupashe upashike sipendi kila siku tuwe sisi tu wanawake. Mbona wanawake wengine tuna akili za mbuzi kuchelewa kujisahau.

Jamani nayasema haya baada ya kustaajabu ya Musa, kuna shoga yangu mmoja aliolewa na mume aliyempenda na kumpa kila kitu. Lakini shoga akili zake alizihamishia chini badala ya kichwani baada ya kupata kidudu mtu. Akawa haoni hasikii baada ya kunogewa, akashinikiza talaka mpaka akapewa. Lakini bahati mbaya alipokwenda pakadunda na huku nyuma bwana kaoa mwingine!

Juzi nilistaajabu kuwaona shostito na mumewe wa zamani wakitoka nyumba ya wageni kufanya mambo yao. Nami kwa umbeya nilipokutana naye nilitaka kujua kulikoni gari lilikuwa lake leo aombe lifti.
“Mmh, Shoga sijui nikuambie nini, mbona najuta akili kuzihamishia chini, sasa hivi nimekosa Bara na Pwani. Kwa kweli bado tunapendana sana, lakini ndivyo hivyo kaoa na kingine familia yake haitaki kuniona kwa vile niliondoka kwa kashfa.”

Shoga zangu mnalo! Si wajinga waliosema ndoa mbaya ukiwa nayo, lakini ukiichezea kuipata tena ni kazi. Kwa nini ufanyie mchezo ndoa yako? Kwa nini umdharau mumeo kwa kibwana cha pembeni? Hata kama si fundi sana kitandani, unatakiwa kumfundisha taratibu ili akupe raha unazozitaka na si kutoka nje ya ndoa kisha urukwe na akili!
Siku zote sigara ya kuokota haiishi hamu lakini ya kununua hukinaisha, hivyohivyo ndani ya ndoa unaweza kumkinai mumeo na kuliona penzi la pembeni tamu, lakini unajisahau kuwa hakuna tofauti zaidi ya akili zako kuzihamishia chini. Unaachwa kwa kulazimisha mwenyewe!

Msichokijua, wanaume wa pembeni wamezoea vya kunyonga, ukiachwa na mumeo na wenyewe wanaingia mitini!. Unataka kurudi kwa mumeo, lakini unaona aibu kwa vile uliondoka kwa kashfa kubwa. Matokeo yake unaanza kumvizia kichochoroni kwa vile bado alikuwa anakupenda, inabidi aisaliti ndoa yake na kupelekana gesti wakati mwanzo alikuwa wako.

Unakuwa kama mtu aliyekuwa anamiliki gari halafu akaligawa bila sababu, kesho unaomba lifti. Jamani tuone aibu kuchezea ndoa zetu, kuolewa bahati, jiulize wangapi wanaitaka ndoa mpaka kwa waganga hawaipati ila wewe unaichezea!

Nina imani mwenye masikio umesikia kama wajifanya kenge kazi unayo.

Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

GPL

No comments: