|
Ubalozi wa Marekani
Dar es Salaam
TANZANIA
|
Mawazo machache wakati Watu wa Marekani
tukielekea katika
uchaguzi wa Rais wetu ajaye
Na Virginia Blaser – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
2 Novemba 2016
Katika miezi michache iliyopita, nimeona
ongezeko kubwa la hamasa nchini Tanzania ya kufuatilia uchaguzi nchini Marekani
na Mfumo wetu wa kipekee wa uchaguzi. Tunapokaribia
Siku ya Uchaguzi hapo tarehe 8 Novemba, tunasherehekea sio tu utamaduni wa kuwa
na chaguzi zilizo huru na wazi ambazo ndizo zimekuwa zikitupatia marais wetu
toka mwaka 1789, bali pia amali zilizokita mizizi zinazowapa raia wote nafasi
ya kuamua kuhusu serikali yao.
Bila kujali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa
Mwaka 2016, mchakato wa kidemokrasia uliodumu kwa muda mrefu tunaoutumia
kuchagua rais mpya, unadhihirisha wazi amali na maadili ambayo sisi, kama
Wamarekani tunayaenzi na kujivunia: uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na
vyombo vya habari, taasisi huru na utawala wa sheria. Maadili haya ndiyo
nguzo ya demokrasia yetu. Kutokana nayo, raia wa Marekani wanaweza kushiriki
kwa uhuru na uwazi kabisa katika mijadala ya kijamii huku wakihakikishiwa kuwa
ushiriki wao kamilifu sio tu unakaribishwa, bali ni sehemu muhimu ya kuendeleza
na kuimarisha nchi yetu.
Waasisi wa taifa letu walihakikisha maadili
haya yanajumuishwa katika Katiba ya Marekani pale walipoanzisha mfumo wa
uchaguzi wa Kura za Majimbo (Electoral College). Japokuwa mfumo wa awali wa
uchaguzi umebadilika kidogo toka kuasisiwa kwa taifa letu, bado tunaendelea
kuutumia mfumo huu wa kura za majimbo ambao hulipa kila jimbo idadi mahsusi ya
kura kulingana na idadi ya watu wake. Ili kushinda uchaguzi kwa kupata kura za
kutosha kuwa rais – angalau kura 270 kati ya kura zote 538 za majimbo, ni lazima
wagombea wajinadi katika masuala mbalimbali yanayowagusa wapiga kura katika
kila jimbo nchi nzima, iwe ni katika majimbo makubwa na hata yale madogo.
Wakati wapiga kura wanakwenda kupiga kura zao,
wanachagua mgombea atakayepata kura nyingi zaidi katika kura za jimbo lao. Waasisi
wa taifa letu waliona kuwa mchakato huu ndio ambao ungehakikisha kuwa sauti za
watu zinasikika na kero zao zinashughulikiwa. Tunaendeleza mchakato huu
kutokana na fursa unaowapatia Wamarekani kujadili maoni na mitazamo yao
mbalimbali kuhusu masuala yanayowagusa.
Kwa kawaida chaguzi za Marekani hujumuisha
kipengele muhimu cha midahalo mikali ya wazi. Kwa hakika, kama Wamarekani
tunathamini sana kuwa na mfumo unaowezesha na kupanua nafasi ya demokrasia,
unaoviwezesha vyama vya siasa kuelezea misimamo na mitazamo yao inayotofautiana
na kuwezesha uhuru wa vyombo vya habari. Mfumo huu ndio unaotuwezesha kushiriki
katika majadiliano makali na ya kina kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa
yanayojenga jamii yetu na mstakabali wetu wa pamoja – wakati wa uchaguzi na
katika maisha yetu ya kila siku.
No comments:
Post a Comment