ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 5, 2018

KENYATTA- HAKUNA ATAKAYEPONA VITA YA RUSHWA

Picha
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameweka wazi kuhusu mapambano dhidi ya mafisadi na wala rushwa kuwa angependa harakati hiyo iwe ndio urithi wake atakaouacha baada ya kumaliza muda wake mwaka 2022.

Katika mahojiano na kipindi cha ‘Hard Talk’ cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) hivi karibuni, Rais Kenyatta alionekana kuiweka vita ya mafisadi na wala rushwa katika ‘chungu’ kimoja na ajenda kubwa nne za chama chake ambazo ni huduma ya afya, nyumba za gharama nafuu, uwepo wa chakula cha kutosha na uzalishaji wa viwanda.

“Hiki ni kitu ambacho nimejitolea kukipigania, ndio urithi wangu ninaotaka kuuacha, yaani vita dhidi ya rushwa na ufisadi ni vitu visivyokwepa, nitahakikisha kunakuwa na uwazi katika kila eneo ili kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika vile inavyotakiwa,” amesema Rais Kenyatta katika mahojiano hayo.

Amesema amejitolea katika vita hiyo na kuiomba mahakama kuharakisha kusikiliza kesi za ufisadi ili hatua za kuwakamata watuhumiwa kuendelea bila kumuonea mtu.

“Kama serikali, kama mimi nimejitolea katika kupambana na wala rushwa na mafisadi tatizo la rushwa na ufisadi ni sawa na mnyama ambaye tumeamua kumchinja. Kilichobaki ni kwa mahakama zetu huru kufanya kazi yao ya kutoa haki kwa niaba ya wananchi wa Kenya,” amesema Kenyatta.

Akielezea vita ya rushwa na ufisadi iliyokuwa inafanyika kimya kimya katika kipindi cha nyuma, Rais Kenyatta alisema kwa sasa hakuna atakayepona kama alikuwa akijihusisha na mambo ya Rushwa.

“Haijalishi wewe ni nani hata kama wewe ni sehemu ya familia yangu, nimesema waliopewa jukumu la kupambana na wala rushwa wako huru kufanya kazi yao,” aliongeza Rais Kenyatta.

Mbali na hilo pia Rais Kenyatta kwa mara ya kwanza alielezea namna alivyoamuru viongozi kufanyiwa ukaguzi wa maisha yao Juni mwaka huu, baada ya kulalamikiwa na wabunge hususani mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi na kwamba kazi hiyo itafanyika hata kwa viongozi waliostaafu hata kufikia wakati wa utawala wa Mzee Jomo Kenyatta. Rais Kenyatta alisisitiza kuwa ukaguzi wa mifumo ya maisha ya viongozi wakubwa serikalini utaendelea akiwemo yeye mwenyewe.

Alisema yeye binafsi hana shaka na utajiri wa familia yake, kwani ni wa kihistoria na kwamba yuko tayari kuchunguzwa kwa hilo.

Familia ya Rais Kenyatta inamiliki ardhi ipatayo ekari 500,000 ambayo ilichukuliwa na baba yake miaka ya 1960 na 1970.

Kutokana na utajiri huo na mali nyingine, mwaka 2011 Jarida maarufu la habari za uchumi la Forbes la Marekani lilimtaja Kenyatta kuwa anashika nafasi ya 26 kati ya watu 40 matajiri zaidi barani Afrika.

Mbali ya utajiri wa ardhi, kitu ambacho ni adimu kwa nchini Kenya, Kenyatta anatajwa kuwa na utajiri wenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 (Sh trilioni 1.05).

Ndiye mmiliki wa kampuni kubwa ya maziwa ya Brookside Dairies, hoteli za Heritage, hoteli za kitalii, sekta ya fedha, sekta ya utalii, shule, kilimo cha kahawa, chai na mkonge, vyombo vya habari vikiwemo kituo cha televisheni cha K24, gazeti la People, vituo vya redio vya Kameme Fm, Meru Fm na Milele Fm, na kadhalika.

HABARI LEO

No comments: