ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 5, 2018

WALIMU KIZIMBANI KIFO CHA MWANAFUNZI

Picha
WALIMU wawili wa Shule ya Msingi Kibeta Manispaa ya Bukoba, Respicius Mtazangira na Herieth Gerald, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba kjibu shitaka la mauaji ya mwanafunzi Sperius Eradius (13).

Washitakikwa hao wamesomewa shitaka la mauaji linalowakabili jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, John Kapogoro.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 18 ya mwaka 2018, washitakiwa hao wawili hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao, bali Mahakama Kuu.

Baada ya kusomewa shitaka linalowakabili walirudishwa mahabusu na kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kimahakama ili iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Kapogoro baada ya washitakiwa kusomewa shitaka ameamuru warudishwe mahabusu kwa kuwa shitaka linalowakabili halina dhamana.

Akitoa ufafanuzi wa kesi hiyo, Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi, Athuman Matuma Kirati amesema, ushahidi wa kesi hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na ofisi yake inaendelea na utaratibu wa kufungua jalada la kesi hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Eradius alifariki dunia Agosti 27, mwaka huu, muda mfupi baada ya kupigwa shuleni Kibeta na Mtazangira aliyekuwa mwalimu wa nidhamu katika shule hiyo kwa kutuhumiwa kuiba mkoba ya Mwalimu Herieth Gerald.

Mwanafunzi huyo alizikwa Agosti 31, mwaka huu nyumbani kwao, kata ya Mubunda, kijiji cha Kitoko wilayani Muleba.

HABARI LEO

No comments: