ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 5, 2018

Polisi yataja sababu ya kumkamata kiongozi wa Chadema



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei
By Godfrey Kahango, Mwananchi gkahango@mwananchi.co.tz

Mbeya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema sababu ya kumkamata mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadia Mwaipalu ni kumuonya yeye na viongozi wenzake dhidi ya maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani na uchochezi wanayoyatoa kwenye majukwaa ya kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio unaoendelea jijini hapa.

Mwaipalu alikamatwa na polisi alfajiri ya kuamkia jana na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kabla ya kupelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RC0) Mkoa wa Mbeya, Modestus kwa ajili ya mahojiano.

Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda Matei alisema licha ya kampeni hizo kuendelea kwa amani na utulivu, zipo taarifa za kiintelijensia za kuwapo kwa matumizi mabaya ya maneno yenye mrengo wa kichochezi yanayotamkwa na viongozi hao kwenye majukwaa ya kampeni.

“Tumemuita huyo bwana Mwaipalu kumsihi yeye na viongozi wake watumie maneno ya staha, maana wamekuwa na maneno yenye mrengo wa kichochezi lakini tulipomhoji basi tumemuachia. Kweli tunazo taarifa za kiintelijensia na wengine tuna ushahidi wa kutosha kuhusiana na maneno wanayoyatoa kwenye majukwaa yao ya kampeni na tumewaita tumewafungulia kesi mahakamani na majalada ya uchunguzi dhidi yao tunaendelea nayo,” alisema kamanda huyo na kuongeza:

“Kumleta mtu kituoni ni utaratibu wetu wa kawaida na huwa tunafanya hivyo pale tunapopata taarifa za kiintelijensia. Na yeye tulimuita ili kumkumbusha kwamba tunahitaji watumie lugha zenye kufuata misingi ya amani na si za uchochezi.”

Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, polisi wataendelea kufuatilia kwa karibu mikutano yote inayoendelea. “Tunawakumbusha wapiga kampeni kuepuka kutoa maneno yanayochochea uvunjifu wa amani, atakayekiuka hata akiwa ni wa CCM tutamuita tu na tayari tulishawahi kumuita kiongozi mmoja wa CCM,” alisema Kamanda Matei.

Akizungumza kwa simu jana, Mwaipalu alisema baada ya mazungumzo aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa leo kuripoti kituoni hapo.

“Wanadai nilipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Mtaa wa Ntundu nilitamka maneno ya kichochezi kuwa tumejipanga kuandaa vijana kutoka wilaya zote siku ya uchaguzi na kama wasimamizi wa uchaguzi watatangaza matokeo tofauti, sisi hatutawaele, kitu ambacho si cha kweli,” alisema.

No comments: