Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola (kushoto) akizungumza na Wananchi wa Kata ya Namhula, Jimboni humo, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo. Lugola alitangaza kufungua miradi mikubwa ya maendeleo jimboni humo hivi karibuni. Kulia ni Mfanyabiashara wa Chakula cha Samaki cha Aluzola, Saimon Katolilo, ambaye aliitwa na Mbunge huyo kutoa elimu kuhusu bidhaa hiyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola akizungumza na viongozi wa Kata ya Muranda, Jimboni humo, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo. Lugola alitangaza kufungua miradi mikubwa ya maendeleo jimboni humo hivi karibuni. Kulia ni Diwani wa Kata hiyo, Jogolo Biswalo, na kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Muranda, Juma Mapole.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola ametangaza kufungua miradi mikubwa mitano ya maendeleo jimboni kwake, Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa katika mikutano yake kwa wananchi wa jimbo hilo siku za nyuma. Lugola amesema tayari mipango imepangwa katika kufanikiwa miradi hiyo inafunguliwa jimboni humo ikiwa ni hatua ya kuondoa umaskini kwa wananchi na kuliletea mafanikio makubwa jimbo hilo na Wilaya ya Bunda kwa ujumla,
Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Namhula, Wilayani humo, leo, Lugola alisema mradi mkubwa wa Maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya kumwagilia mazao mbalimbali ikiwemo zao la mpunga katika Bonde la Namhula tayari wataalamu wamefika kulipima bonde hilo pamoja na kuanza mchakati wa mradi huo, pia uwepo wa maji hayo yatasaidia kumwagilia mazao mengine ya nafaka jimboni humo.
“Mradi mwingine ni wa ufugaji wa kuku wa kienyeji na tuna mashine kubwa za kuangulia vifaranga, maandalizi yapo tayari na eneo la ufugaji huo utakua shule ya Msingi Magunga Kata ya Neluma, pia mradi wa ufugaji wa ng’ombe nyati na ufugaji huo pia utafanyika Sekondari ya Neluma katika Kata hiyo hiyo, na pia tutakuwa na ufugaji wa samaki katika mabonde,” alisema Lugola.
Lugola alisema miradi hiyo itaanza mwakani 2019 na maandalizi yapo tayari na wananchi wawe tayari kuipokea kwa mikono miwili ili iweze kusonga mbele na maendeleo ya jimbo hilo yawe mfano kwa majimbo mengine nchini. “Ndugu wananchi wa jimbo hili, miradi hii ni mikubwa, niliwaahidi na sasa ipo mbioni kuanzishwa, ninachokiomba musiiharibu, muilinde na pia ilete maendeleo ya jimbo letu,” alisema Lugola.
Aidha, Waziri Lugola aliwataka wananchi wa jimbo hilo waanze maandalizi ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuepuka janga la njaa lisije liwakumba endapo hawatalima. Hata hivyo, kijiji hicho alichokitembelea, kwa mujibu wa taarifa ya mipango yao ya kilimo walisema kuwa wana upungufu mkubwa wa mbegu za mazao mbalimbali hasa zao la pamba.
“Ndugu wananchi, nimeagiza maafisa ugani waje kuangalia upungufu wa mbegu za pamba na kutatua kero hii kutokana na taarifa yenu ya mpango wa kilimo ya mwaka huu 2018/2019, na pia nasisitiza zaidi mulime mazao ya chakula kwa wingi,” alisema Lugola. Lugola ameanza ziara jimboni kwake akisikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya pamba, mahindi, mpunga, viazi na mengineyo ambayo wakazi wa jimbo lake wanalima mazao hayo kwa wingi.
No comments:
Post a Comment