Dodoma. Ndege iliyokuwa itue katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma nchini Tanzania leo Alhamisi Machi 5, 2020 imeshindwa kufanya hivyo kutokana na hali ya hewa.
Mapema abiria waliokuwa wakitokea jijini Dar es Salaam kwa ndege za Kampuni ya Precision imeshindwa kutua na hivyo kuilazimu kurejea Dar es Salaam baada ya kuzunguka katika anga la Dodoma kwa dakika kadhaa.
Ndege hiyo zilitakiwa kutua Dodoma kati ya Saa 1.00 na 2.30 asubuhi kwenye uwanja huo.
Alipoulizwa kuhusu tatizo hilo, Meneja Uwanja wa Ndege wa Ndege, Bertha Bankwa amekataa kuzungumza na kutaka yatafutwe mashirika yanayotumia kiwanja.
“Mimi siwezi kuzungumzia mashirika ya hayo ya ndege kwa hiyo ukiwatafuta hao watakwambia shida ni nini hadi ndege zimeshindwa kutua,”amesema.
Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Precision nchini, Sara Waziri amesema ndege yao na nyingine zilizokuwa zitue jijini Dodoma asubuhi zimelazimika kurudi Dar es Salaam.
Amesema wataanza safari ya kurejea Dodoma hali hewa itakapokuwa sawa.
“Kurudi kwa ndege hii Dar es Salaam kunaligharimu shirika upande wa mafuta lakini pia na muda,”amesema.
Ndege hizo hutua katika kiwanja hicho mara mbili kwa siku asubuhi na jioni.
No comments:
Post a Comment