Friday, April 17, 2020

MGODI WA BARRICK BUZWAGI WATOA MSAADA WA VIFAA KUKABILIANA NA CORONA SHINYANGA

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akiishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuiunga mkono serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Afya na Usalama mgodi wa Barrick Buzwagi, Dkt. Antoinette George. Picha na Malunde 1 1 Blog 


Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Barrick kupitia Mgodi wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama imetoa msaada vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 48 kwa ajili ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ‘Covid 19’ katika mkoa wa Shinyanga.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo Ijumaa Aprili 17,2020 na Mkuu wa Kitengo cha Afya na Usalama mgodi wa Barrick Buzwagi, Dkt. Antoinette George kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.

Dkt. Antoinette amevitaja vifaa walivyotoa kuwa ni pamoja na Matanki ya kuoshea mikono ‘washing container set’ 88,goggles 40,Impermiable suits 40,Barakoa (face masks) 400, Vipimia joto (contact less thermometer) 6, Hand wash unit,Chlorine powder na chemical gloves jozi 50.

Dkt. Antoinette amesema Kampuni ya Barrick iko bega kwa bega na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona ndiyo maana imechangia vifaa hivyo ili kuwakinga wananchi dhidi ya Corona.

“Kinga ni bora kuliko tiba .Tumekabidhi vifaa vya kujikinga na Corona kwa Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ili vikatumike kukabiliana na Corona katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo masoko,vituo vya mabasi,minada,vituo vya afya na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Corona”,amesema Dkt. Antoinette.

“Leo tumekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 48 lakini Kampuni ya Barrick imetoa jumla ya shilingi Bilioni 4 zingine kukabiliana na Corona nchini Tanzania ambapo mkoa wa Shinyanga umetengewa shilingi milioni 600”,ameongeza Dkt. Antoinette.
Akipokea vifaa hivyo,Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuiunga mkono serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona huku akibainisha kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

“Tunawashukuru sana Barrick Buzwagi kwa mchango wenu,tutavigawa vifaa hivi katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga ili kama atapatikana mgonjwa basi tuweze kuokoa maisha ya mgonjwa.Maandalizi haya tunayafanya kama binadamu lakini tuendelee kumuomba Mungu atuepushie ugonjwa huu na tuwaombee waliopata maambukizi wapone ili maambukizi yasiwepo”,amesema Telack.

“Kila mtu achukue tahadhari,kunawa mikono maji safi yanayotiririka na sabuni ndiyo silaha yetu kubwa, ambayo tunajivunia, nawa ukiwa nyumbani, nawa ukiwa katika biashara zako,nawa ukiwa kazini,nawa kila wakati” ,amesema

Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za wageni wanaofika katika maeneo yao huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaoleta mzaha kuhusu ugonjwa wa Corona.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha amesema sasa wananchi wengi wana muamko wa kutosha kuhusu ugonjwa wa Corona na kwamba changamoto bado ipo kwenye maeneo ya Baa na Klabu ambazo zinaendelea kukusanya watu pamoja na waendesha bodaboda wanaopakiza watu zaidi ya mmoja ‘mishikaki’

No comments: