ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 1, 2020

Chadema yawataka wabunge wake kutohudhuria bunge


Mwandishi Wetu, Mtanzania

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewaelekeza wabunge wake wote kutohudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea jijini Dodoma ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambapo pamoja na mambo mengine pia amelitaka bunge kusitisha vikao kwa muda wa siku 21 na kuwapima wabunge wote na familia zao ili kubaini ni wangapi wameambukizwa virusi hivyo.

Mbowe amesisitiza wabunge hao kukaa mbali na majengo ya bunge ya Dodoma na Dar es salaam ili kuzuwia kusambaa kwa virusi hivyo.

“Tunalitaka Bunge lisitishe shughuli za bunge kwa siku 21 kuruhusu wabunge na watumishi wote kwenda karantini, kupima wabunge wote na watumishi wa bunge na familia zao kubaini ni wangapi wana maambukizi ya corona ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Licha ya kuwataka wabunge wa Chadema kutohudhuria bungeni, tunawasihi wabunge wengine wote wa vyama vingine kutafakari kama kweli ni salama kuendelea na vikao vya Bunge katika mazingira yaliyopo,” amesema Mbowe kwenye taarifa yake aliyoitoa leo Ijumaa Mei Mosi.

Amesema kamati mahususi za bunge, hususan Kamati ya Huduma za Bunge na Kamati ya Uongozi zinapaswa kufanya vikao vyake kwa njia ya mtandao ili maamuzi muhimu kuhusu utawala wa mwenendo wa bunge yaweze kufanyika.

Aidha, amewasisitiza Watanzania wote kuwa mstari wa kwanza kujikinga na virusi hivyo akidai ni uzembe kusubiri kufanyiwa kinga na mwenzako.

Hatua hiyo inakuja wakati bunge hilo likiomboleza vifo vya wabunge watatu waliofariki dunia katika kipindi cha chini ya wiki mbili ambapo miongoni mwa wabunge hao ni pamoja na Dk. Augustine Mahiga aliyepoteza maisha asubuhi ya leo

No comments: