MUASISI na Mwanzilishi wa Soka la wanawake, Alhaj Dr Maneno Tamba, amefarikia dunia leo Ijumaa saa 8 mchana muda mchache baada ya swala ya saa 7 mchana.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mjumbe wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Chikolo amesema, marehemu amekutwa na umauti katika Hospitali ya Tabata Islamic, jijini Dar es Salaam.
Chikolo amesema, baada ya kutoka msikitini alipokea simu kutoka kwa mjumbe mwenzake juu ya taarifa za msiba wa Mwenyekiti wao.
Muasisi wa soka la wanawake Tanzania aitaka heshima yake akiwa hai
Amesema baada ya taarifa hiyo alilazimika kumpigia simu kijana wa marehemu ambaye alikiri kutokea kwa kifo hicho.
"Muda mchache tu baada ya swala ya saa 7, ndipo amepoteza maisha kiongozi wetu huyu inauma sana msiba wetu sote huu," amesema Chikolo
Amesema marehemu alikuwa akisumbuliwa na Kisukari, Presha, Moyo na Maralia ambayo imemsumbua ndani ya wiki moja mpaka mauti inamkuta.
Amesema baada ya kujiridhisha na taarifa hizo ilimbidi aende msikiti wa Mburahati kutoa taarifa kwa imamu ili atoe tangazo ambapo mwili wa Dr Tamba utazikwa leo Ijumaa saa 12 jioni kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Wanamichezo wamlilia
Mchezaji aliyekulia mkononi mwa muasisi huyo Asha Rashid 'Mwalala' amesema amepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na baada ya kupata taarifa ilimlazimu kufika Tabata ulipo msiba wa kiongozi huyo maarufu hapa nchini.
"Sijaamini mpaka sasa ila ndio kazi ya Mungu katangulia sisi tunafuata niko Tabata msibani huku,"anasema
Mchezaji mwingine aliyepita mikononi mwa Dr Tamba amesema; "Kama sio Dr Tamba nisingekuwa Mwanahamisi mnayeniona leo, huyo mzee ni kila kitu kwangu, nashindwa cha kufanya,"amesikika akilia akakata simu.
Naye Mkurugenzi wa benchi la Mlandizi Queens, Miraji Adam ambaye amewahi kuwa kocha wa Mburahati Queens, amesema soka la Wanawake limepata pigo kuondokewa na mtu mwenye mchango mkubwa.
"Amefanya mambo mengi katika soka la wanawake, ni miongoni mwa walioanzisha ligi ya mkoa wa Dar es Salaam ya wanawake, alikuwa mwenyekiti wa cha soka cha mkoa,"
"Ni mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Yanga Princess, msiba wake umeumiza," amesema.
Kwa upande wa kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi amesema Tamba amefanya mengi na ameacha alama kwenye soka la wanawake itakayoendelea kuishi.
"Hakuna asiyejua kuhusu mchango wa Tamba katika soka la wanawake, tutaenzi aliyoyafanya kwa vitendo kuhakikisha tunafika mbali katika soka la wanawake,"amesema.
Kiungo wa Yanga Princess, Fatuma Bushiri 'Tshishimbi' amesema Tamba ana mchango mkubwa katika soka la wanawake kufikia hatua ya kuthaminiwa na jamii.
"Atakumbukwa kwa mengi hata nikiyataja siwezi kuyamaliza kaacha alama inayoishi, katangulia ni safari ya kila mmoja," amesema.
No comments:
Post a Comment