ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 1, 2020

Kipa Simba afichua alivyoteswa na ushirikina

By CHARLES ABEL Mwanaspoti

KIPA wa zamani wa Simba, Daniel Agyei amefichua kuwa nusura masuala ya kishirikina yakipoteza kipaji chake hapo nyuma na kueleza kwamba aliokolewa na nguvu za Mungu.

Agyei (30) anayedakia Seneta Kenema ya Ethiopia kwa sasa amesema kuwa alikumbana na balaa hilo mara baada ya kuitumikia timu ya Taifa ya Ghana katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini.

"Nachukia kuzungumzia masuala hayo lakini naamini huu ni wakati wa kuyaweka hadharani ili kizazi kinachokuja kijue kinakabiliana nayo vipi pindi yakiwatokea.

"Nimepitia changamoto nyingi baada ya Kombe la Dunia mwaka 2010. Mambo yaliniendea kombo na kiwango changu kwenye ligi kiliporomoka vibaya. Niliamini ni uchovu lakini watu pembeni wakaanza kuniambia kuhusu masuala ya ushirikina ambayo awali kuna mchungaji alinigusia na kuniambia kuwa nimefanyiwa ushirikina.

"Mchungaji aliniambia kuwa kuna watu wanapambana ili waniangushe chini, nisiende nje ya nchi kucheza soka la kulipwa lakini nilimuomba Mungu na kuwa na imani kuwa nia yao itashindwa. Na kwa vile mimi ni mtu wa maombi sikuwa na wasiwasi kwa hilo ingawa kilichonipa hofu ni kwamba pengine wahusika wangewadhuru ndugu zangu," amesema Agyei alipokuwa akihojiwa na kituo cha luninga cha CK nchini Ghana.

Kipa huyo amesema kuwa hayo yalimkuta akiwa anacheza Ghana kabla ya kufunga safari hadi Simba alikochezea kwa msimu mmoja tu wa 2016/2017 na kutimkia zake Ethiopia alikojiunga na Jimma Aba Jifar na baadaye kujiunga na Kenema aliyopo sasa.

"Nimekuwa ninaishi nikimtegemea Mungu lakini masuala kama hayo ifahamike kuwa yapo ingawa kwa mchezaji hapaswi kuyatilia maanani na badala yake akili anapaswa kuielekeza uwanjani," amesema Agyei.

Kauli hiyo ya Agyei imekuja siku chache baada ya aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan kukiri hadharani kuwa amewahi kushiriki masuala hayo siku za nyuma.

"Kabla ya kuingia uwanjani tulikuwa tunapewa maji tuoge. Ni jambo ambalo wote tulitakiwa kufanya na iwapo ukikataa, tukifungwa watu wanakushushia lawama wewe ambaye hukuoga kuwa umesababisha tupoteze mechi," alisema Asamoah.

Hata hivyo, Asamoah alisema kuwa mara baada ya kuanza kuingia katika soka la weledi, aliachana na imani hizo ambazo zimeshika kasi katika maeneo mbalimbali barani Afrika

No comments: