KUJIFUNZA, kuelewa na kufuata ni kitu kizuri kwa mtu mwenye hulka ya kupanua mawazo yake. Hakuna aliyekamilika, siku watu wanakosea. Hakuna mtaalamu wa kudumu wa mapenzi.
Kwenye mapenzi tunazidiana uelewa tu. Hapa kwenye All About Love, ni mahali sahihi pa marafiki kukutana na kubadilishana mawazo. Wengi wamenufaika kwa kuwa wadau wa kona hii.
Ni safu ya kitambo iliyobadilisha fikra za wengi. Nashukuru wale ambao wananishirikisha mafanikio yao ya kimapenzi baada ya kusoma mada zangu na kuzifanyia kazi.
Marafiki, leo nahitimisha mada hii kabla ya kuanza kuchambua mpya wiki ijayo.
Ni kuhusu wanawake wanavyopotezewa muda na wanaume ambao hukaa nao muda mrefu katika uchumba unaishia hewani.
Nilifafanua kwa undani mambo mawili; kuachwa kwa muda mfupi na wanaume tofauti – nikaeleza sababu na namna ya kufanya. Pia nilifafanua kuhusu kuachwa kwa wasichana baada ya kukaa muda mrefu kwenye uhusiano.
Kama mtakumbuka, nilisema si sahihi sana kukaa kwenye urafiki kwa muda mrefu. Usidanganyike na pete, mwenzi wako anaweza kubadili mawazo wakati wowote. Uchumba wa muda mrefu lazima uwe na sababu maalum, labda masomo n.k.
Kama umepata mchumba, kuna mambo muhimu tu ambayo ukiyachunguza na kujiridhisha, mnatakiwa kuingia kwenye ndoa, bila kusubiri zaidi. Hebu tuone mambo hayo.
MAMBO YA MSINGI KUCHUNGUZA
(i) Unampenda kwa dhati?
Tiketi ya kwanza kwenye uhusiano ni kupenda. Lazima ujihakikishie kuwa mwanaume uliye naye unapenda na nafsi yako imeridhika.
(ii) Anakupenda?
Chunguza kama anakupenda. Yapo mambo ya msingi ambayo yakionekana utakuwa na hakika kuwa mwanaume wako anakupenda kwa dhati.
Kwanza namna ambayo anapenda ukaribu wenu, anavyokushirikisha kwenye mambo yake, kukujali. Mfano unaumwa, anakuwa karibu na wewe na wakati mwingine hukuchukua na kukupeleka hospitalini kutafuta tiba.
Atapenda kujua kuhusu ndugu zako, hali zao kiafya na mengine ya msingi. Mwanaume wa ukweli, ambaye anakupenda, atahakikisha yeye anakuwa faraja yako na kukuongoza siku zote.
Akiwa na tabia hii maana yake anakupenda.
(iii) Dini.
Lazima kuangalia suala la dini. Inashauriwa wanaooana wawe wa madhehebu moja ili kuepusha migongano. Mambo ya kiroho yana uhusiano mkubwa sana kwenye ndoa.
Imani husaidia zaidi kutatua migogoro, matatizo ya kuua nk. Haitakuwa jambo zuri, mpate watoto ambao hawatajua wapi panawafaa kuabudu.
Yapo madhehebu yanayoruhusu ndoa za mseto lakini kwa baadaye inaweza kuleta usumbufu. Zungumzeni, kama ni lazima kuoana, mmoja wao akubali kuhamia kwa mwenzake (tena kwa kuamini, si kwa ajili ya ndoa).
(iv) Mila.
Chunguza mila za kabila lao. Jaribu hata kuwatumia wazee. Kuna baadhi ya makabila yana mila ambazo kwa wengine zinakuwa na migongano. Kuwa na hakika na hilo kwanza.
YA NINI KUPOTEZA MUDA?
Baada ya kuchunguza yote hayo na kujihakikishia, una sababu gani ya kupotezewa muda? Kama umeridhika na hayo, maana yake mnatakiwa kukaa na kujadili kuhusu ndoa, kama hataki ujue si wako.
Ni uamuzi wako mwenyewe, kuamua kupotezewa muda au kuwa makini na maamuzi yako. Ndugu yangu kila kitu kipo vichwani mwetu. Tumepewa uwezo wa kufikiri wote, tatizo ni namna ya kufikiri tu. Shughulisha ubongo wako.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
No comments:
Post a Comment