Advertisements

Thursday, July 22, 2021

MUME AUA MKE SINGIDA AKIOMBWA HELA YA ADA YA MTOTO

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo mkoani hapa leo hii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) misokoto ya bangi iliyokamatwa na jeshi hilo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MWANAMKE mmoja Moshi Mkimbu (40) mkazi wa Kijiji cha Ndulungu Tarafa ya Ndago Wilaya ya Iramba mkoani Singida ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali na mume wake aitwaye Juma Shabani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa akizungumza na waandishi wa habari leo aamethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Julai 18, 2021 katika kitongoji cha Misughaa na kuwa mtuhumiwa alikamatwa na atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.

Mutabihirwa alisema kuwa uchunguzi wa awali wa Jeshi la polisi umebaini kuwa chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia pamoja na ulevi baada ya marehemu kudai pesa za mahindi yaliyouzwa kwa ajili ya ada ya mtoto shuleni, ndipo mume wake huyo alianza kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na kitu chenye ncha kali na kusababisha kifo cha mke wake.

Katika tukio lingine alisema jeshi hilo mkoani hapa linaendelea na misako mbalimbali ya kubaini uhalifu kutokana na mikakati iliyojiwekea ya kuweka mkoa wa singida salama ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu Aprili hadi Julai 2021, Jeshi la polisi limefanya misako na kufanikiwa kukakamata dawa aina bhangi misokoto 757 watuhumiwa tisa (9), watuhumiwa saba kesi zipo mahakamani hatua ya kusikilizwa na watuhumiwa wawili wametiwa hatiana.

Alisema mtuhumiwa mmoja wa dawa za kulevya aina heroine kete moja alikamatwa na kesi ipo mahakamani na Pombe ya moshi (gongo) lita 113 zilikamatwa na watuhumiwa 24 ambapo watuhumiwa walifikishwa mahakamani.

“Kesi 16 watuhumiwa walitiwa hatiani na watuhumiwa 8 kesi bado zinaendelea mahakamani hatua ya kusikilizwa na pia pikipiki moja aina ya SANLG ilikamatwa baada ya pikipiki hiyo kuporwa na mtuhumiwa mmoja ambaye alikamatwa na alifikishwa mahakamani na tayari amehukumiwa kutumikia jela mwaka mmoja,” alisema.

Mutabihirwa ametoa shukrani kwa wananchi na raia wema kwa kutoa ushirikiano na kupata mafanikio hayo hivyo wito wa jeshi hilo kwa wananchi wote hususani wanandoa kuacha tabia na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika familia zinazo wazunguka na kuwatengemea kwani vitendo hivi hupelekea madhara makubwa na kusababisha vifo katika jamii.

Aidha Mutabihirwa amewataka wananchi kuacha tabia ya ulevi uliopindukia na matumizi ya dawa kulevya bali waishi kwa amani, furaha na kufuata sheria za nchi na pindi matatizo ya kifamilia yanapotokea wafike kwenye vituo vya Polisi kwenye madawati maalumu ya kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto na si kujichukulia sheria
mkononi.

No comments: