ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 1, 2021

SERIKALI YAIAGIZA TIPER KUTOA TAARIFA ZA UENDESHAJI KAMPUNI KWA WAKATI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipotembelea Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja wakati alipotembelea Kampuni hiyo iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja akitoa maelezo kuhusu utendaji wa Kampuni ya TIPER kufuatia ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali kwenye kampuni hiyo tarehe 31 Julai, 2021.
Watumishi wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali alipokuwa akizungumza nao (Hayumo pichani) alipotembelea kampuni hiyo ya TIPER tarehe 31 Julai, 2021.

Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam

Serikali imeiagiza Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) kuhakikisha inatoa taarifa za uendeshaji wa kampuni hiyo kwa wakati, ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza baadaye kutokana na kutokutoa taarifa kwa wakati.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake kwenye kampuni hiyo iliyolenga kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni ya TIPER.

Katika ziara yake, Naibu Katibu Mkuu Mahimbali, ametembelea kwenye maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta jambo ambalo ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja, ameishukuru Serikali kwa kufika katika eneo hilo ambapo wameweza kukubaliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa kwa wakati.

Amesema, licha ya mafanikio waliyonayo, bado kuna changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa kuharibika kwa vifaa vya kusukuma mafuta pindi wanapoyatoa kwenye meli, vifaa ambavyo havipatikani nchini hadi viagizwe nje ya nchi.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali amesema, endapo taarifa hizo zitatolewa mapema, itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo.

Ziara hiyo ni mwanzo wa ziara nyingine katika taasisi zote zenye ubia na Serikali katika Sekta ndogo ya Mafuta hapa nchini kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali, aliambatana na baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini Tanzania (EWURA) na Kampuni ya Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta nchini (TANOIL).

No comments: