ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 1, 2021

WAZIRI CHAMURIHO AWATAKA WAHANDISI KUCHANGAMKIA FURSA YA MIRADI

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho amewataka wahandisi washauri kuchangamkia fursa zinazotolewa katika miradi ya kielelezo hapa nchini, ili kuweza kukua kitaaluma na kukuza uchumi wa Taifa.

Alitoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa 35 wa mwaka wa wahandisi washauri ulioandaliwa na Umoja wa Wahandisi Washauri (ACET), mkoani Dar es Salaam uliobeba kaulimbiu ya uhusikaji wa wahandisi washauri wazawa katika miradi ya kielelezo.

Dk. Chamuriho alisema: “kuhusika kwa wahandisi washauri katika miradi kunasaidia kuendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2020-2025 ya kuwa Taifa la uchumi wa kati wa chini kwa miaka mitano kabla ya wakati wake”

Aliongeza: “Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yanahusishwa na ninyi wahandisi kwani miradi hii ndiyo inayoleta mafanikio makubwa katika uendelezaji wa miundombinu ambayo ndiyo chachu ya ukuaji wa uchumi”

Alisema ni jukumu la wahandisi kuhakikisha miradi mikubwa ambayo ni ya kielelezo inatendewa haki kwa weledi na kuzingatia thamani ya fedha, ili kuleta tija kwa taifa na kuwawezesha kupata fursa zaidi katika miradi inayotekelezwa hapa nchini.

Aidha, aliwakumbusha wahandisi hao kuwa sayansi na teknolojia vinakuwa kwa kasi, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanajijengea uwezo ili kuendana na kasi hiyo kwa kuhudhuria kozi mbalimbali zinazotolewa ndani na nje ya nchi.

Kuhusu changamoto za kutoaminiwa katika utekelezaji wa miradi mkubwa, Dk. Chamuriho alisema Serikali imeweka sera yenye mambo makuu matatu ambayo ni kujenga uwezo wa upatikanaji wa masoko, kupiga chapuo kwanye teknolojia ili kukuza wakandarasi wazawa.

“Sera hii ya ndani inawezesha makandarasi wa nje kuwahusisha makandarasi wa wazawa ili kuweza kuwainua hivyo hakikisheni mnazijua sera hii ya ndani, Sheria ya Manunuzi ya umma pamoja na kanuni zake ili muweze kuzitekeleza,” alisema Dk. Chamuriho

Alisema ili kuwafanya wahandisi washauri waweze kuaminiwa zaidi ni vema wakajiunga ili kuweza kutengeneza kampuni kubwa zenye uwezo wa kutekeleza miradi kwa weledi zaidi.

Naye Rais wa Umoja wa Wahandisi Washauri (ACET), Mhandisi Deogratius Mugishagwe, aliiomba serikali kuhakikisha wahandisi wanahusishwa katika mpango wa maendeleo wa serikali wa miaka mitano pamoja na kuwawezesha kulipwa kwa wakati kwa kupanga miradi inayotekelezwa kwa kufuata vipaumbele.

Alisema changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni pamoja na kuingiliwa na watu wasiokuwa na ujuzi wa fani, kuchelewa kwa malipo.

Mugishangwe alisema ACET wanachokifanya ni kuhakikisha wahandisi washauri wanajengewa uwezo kila wakati ili waweze kuwa na uwezo wa kushindana na wahandisi washauri kutoka nje ya nchi.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

No comments: