Saturday, May 7, 2022

FEDHA ZA MIRADI YA AFYA ZITUMIKE KWA UMAKINI- MAJALIWA



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Mradi wa USAID AFYA YANGU kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright , Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha bango baada ya kuzindua Mradi wa USAID AFYA YANGU kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mradi wa USAID AFYA YANGU kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 6, 2022.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza rasilimali zote zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya zitumike kwa uangalifu na uaminifu ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanatekelezwa na kuleta tija kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo (Ijumaa, Mei 6, 2022) wakati akizindua mradi wa USAID Afya Yangu ama Comprehensive Client Centered Health Program (C3HP) unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania).

“Mamlaka za Serikali za Mitaa toeni ushirikiano wote utakaofanikisha utekelezaji wa mradi huu kwa mafanikio. Watendaji wabadhirifu wasipewe nafasi kuhujumu mradi huu. Viongozi, fuatilieni mara kwa mara ili kuhakikisha malengo ya mradi yanatekelezwa na kuleta tija.”

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, hivyo imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya afya kwa kutekeleza mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma. “Mojawapo ya vipaumbele ni mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.”

Waziri Mkuu amesema kuwa jitihada mbalimbali za Serikali pamoja na wadau zimeanza kuzaa matunda, ambapo katika kutekeleza mkakati wa kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kiasi kikubwa kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 13.5 mwaka 2015 hadi asilimia saba mwaka 2020.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kupambana na vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga kwa kutekeleza Mpango wa Kuimarisha Afya ya Msingi. “Mpango huu ulitutaka kuongeza vituo vya afya ili kila kata iwe na kituo cha afya.”

“Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya vituo vya afya 487 na hospitali za wilaya 102 zimejengwa au kukarabatiwa ili kutoa huduma za afya ya msingi ikiwemo ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, haya ni mafanikio makubwa sana.”

Amesema ongezeko la vituo hivyo linaifanya Tanzania kuwa kati ya nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara ambazo zimefikia kwa kiasi kikubwa vigezo vya Umoja wa Mataifa vya Utoaji Huduma za Dharura za Uzazi na Mtoto Mchanga.

Ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za dharura kwa kuzingatia idadi ya watu na jiografia ya maeneo, kiwango kikubwa cha akinamama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma na kiwango cha kuridhisha cha wajawazito.

Akizungumzia kuhusu mradi wa USAID Afya Yangu amesema amefurahishwa sana na mradi huo ambao una nia ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma ya afya ya uzazi hapa nchini ambao unalenga kumuwezesha mtu binafsi aweze kuimarisha uwezo wake wa kuwa na tabia chanya katika kuzingatia mahitaji ya afya yake.

Malengo mengine ni kumuwezesha mtu kujihudumia mwenyewe pamoja na upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwa mtu binafsi. Pia, umelenga kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi na mtoto.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) imetoa ufadhili wa miradi mitatu ya USAID Afya Yangu kwa Mashirika ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Jhpiego, Deloitte kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa Comprehensive Client Centered Health Program (C3HP) unaotekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba 2021 hadi Oktoba 2027.

Pia, Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika kutoa ufadhili wa utekelezaji wa afua za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, pamoja na Afya ya Mama na Mtoto zitakazokuwa zinatekelezwa na miradi hiyo ya USAID Afya Yangu ambayo wanufaika wa mwisho kabisa ni Watanzania hasa wale walio maeneo ya pembezoni ya mikoa ambayo miradi hii itatekelezwa.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright, amesema urafiki na Ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani umeendelea kukua na kuimarika siku hadi siku jambo ambalo linachangia Ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Nchi ya hizo.

“Marekani imeendelea kuwa rafiki na mdau mkubwa wa maendeleo kwa Watanzania, uzinduzi wa mradi huu ni kithibitisho cha namna ambavyo tumejikita katika kuhakikisha tunashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya Watanzania katika Sekta za Afya, Miundombinu, na Uchumi.”

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri alisema USAID Afya Yangu ni programu ya miaka mitano, inayojumuisha miradi itakayoshughulikia masuala ya VVU, Kifua Kikuu, Uzazi wa Mpango, Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina takriban watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, inakabiliwa na changamoto za afya ya uzazi, watoto wachanga na vijana na inaendelea kuwa na kesi za UVIKO-19 ambazo zimeathiri makundi hatarishi kama vile akina mama wajawazito na watu wanaoishi na VVU.

"Serikali ya Marekani imedhamiria kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ngazi ya Serikali kuu na mikoa kutoa huduma bora za kinga, matunzo na matibabu ya VVU.

No comments: