Advertisements

Monday, May 29, 2023

MAMLAKA KAMILI NJIA PEKEE YA MAFANIKIO ZANZIBAR - MHE. OTHMAN

 Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema wanachokihitaji Wazanzibari ni Mamlaka Kamili ya kuwawezesha kuishi kama raia huru wenye thamani ndani ya Nchi yao.


Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo akihutubia Mkutano wa Hadhara wa Chama chake, huko Viwanja vya Garagara, Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.

Amesema kuwa mahitaji ya Wazanzibari waliopo ndani na hata nje ya Nchi, ni kuona Zanzibar inasonga mbele kimaendeleo na kujiamulia mambo yake ambapo hayo siyo rahisi kuyafikia pasi na kuwepo Mamlaka Kamili ya kujiendesha.

Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa kabla ya kuunganishwa na Tanganyika mnamo mwaka 1964, Zanzibar ilikuwa ni Jamhuri huru iliyokuwa na mamlaka kamili ya kujipangia na kujisimamia mambo yake yenyewe. Amesema mfumo uliokuja wa Muungano ulikuja kufifiliza mamlaka hiyo, na pia kunyima uhuru, heshima na thamani ya Wazanzibari.

Makamu Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo amesema mfumo wa Muungano uliopo umefanya hata isijulikane jambo lipi ni la Muungano na lipi silo. Akitoa mfano, alisema leo Zanzibar inasema inaujenga upya Uwanja wa Amaan lakini haina uwezo wa kushiriki mashindano ya michezo ya kimataifa wakati michezo si jambo la Muungano.

Hivyo amesema kinachohitajika sasa ni kujiandaa, kushikamana na kuitumia fursa iliyopo kupitia Mchakato ujao wa Katiba Mpya na pia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, utakaopelekea kuunda Muungano wenye heshima kwa pande zote, sambamba na kuirejeshea Zanzibar Mamlaka Kamili, ambayo yatapelekea Wazanzibari kuishi katika Nchi yao wakiheshimika na kuwa na thamani inayostahiki.

"Tunaposema Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili tunakusudia kujenga Misingi ya Nchi na maisha ya wananchi na ili kumpa Mzanzibari thamani yake katika Nchi yake, na wala siyo kumbagua", amesisitiza Mheshimiwa Othman.

Akisisitiza kuhusu uwazi Mhe. Othman amesema ACT Wazalendo itaendelea kuhoji matumizi ya fedha za umma kwani ni wajibu wake kuwasemea wananchi. Alisema, "Fedha za Serikali ni mali ya Umma na sio mtu binafsi, hivyo matumizi yoyote yanayohusu fedha za umma yanahitaji uwazi na uadilifu mkubwa zaidi kwa maslahi ya Nchi na wananchi wenyewe."

Awali akizungumzia Zanzibar Mpya inayokusudiwa kujengwa na ACT Wazalendo, amesema ni ile ambayo watu wake wote watatendewa sawa bila ya kubaguliwa. Ameongeza kwa kusema, "Wazanzibari wamekosa haki ya kutambuliwa Nchini kwao, huu ni uonevu wa hali ya juu, kiliopo hapa ni haki ya ukaazi tu ambayo nayo wapo wananchi wananyimwa".

Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuhutubia, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Ndugu Ismail Jussa, amekosoa Serikali ya  Awamu ya Nane ya Zanzibar akisema imekuwa ikiendelea kutoa ahadi kwa wananchi kama vile bado nchi iko katika Kampeni za Uchaguzi. Alisema hakuna linalotekelezwa na hiyo inaashiria kushindwa na uendeshaji wa nchi huku gharama za maisha zikizidi kupanda na mambo yakizidi kuwawiya vigumu wananchi.

Amehoji pia gharama za Ukarabati unaoendelea wa Uwanja wa Amaan Zanzibar, na vigezo ambavyo Serikali imevitumia kuwapata wazabuni waliopewa kazi hiyo.

Kwa upande mwengine alihoji msingi wa ubinafsishaji wa uendeshaji wa Bandari ya Malindi na utaratibu uliotumika kufikia maamuzi hayo. "Serikali ilisema Mapato ya Bandari yameongezeka tangu iingie Awamu hii, sasa leo tunasikia Shirika la Bandari linakodishwa kwa Muwekezaji ili aliendeleze, je kuna haja gani ya kumpa mgeni kuliendeleza ilhali tumeambiwa uongozi wa Shirika wawanakwenda nalo vyema?", ameendelea kuhoji Jussa.
Kwa upande wake, Mshauri wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Bw. Mansoor Yussuf Himid, amegusia Ukarabati wa Barabara ya Uwanja wa Ndege kuelekea Mnazi Mmoja, Kisiwani hapa akisema, "inadhihirisha uharibifu wa fedha za umma, kwani ni wazi bado inapitika na ina kiwango, bali yapo mahospitali mengi mapya na ya zamani ambayo hayana madawa wala vitendea kazi na hayapewi kipaumbele".

Katika salamu zake, Mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi A kichama, Bi. Raisa Abdallah Mussa, naye amehoji akisema, "ni ajabu kuona yale mambo ya asili yaliyoasisiwa na Wazee wetu ikiwemo Uwanja wa Amaan unabadilishwa kwa  kuvunjwa kwa madai ya kuboreshwa, kwanini wasijenge tu mwengine na ule ukabakia na kuendelezwa kama ulivyo ili kutoa fursa zaidi ya maendeleo ya michezo kwa vijana wetu?".

Huo ni mfululizo wa mikutano  ambayo inalenga kile kilichoelezwa kwamba ni kuufahamisha umma wa wananchi juu ya Sera Mpya ya Chama hicho isemayo, 'Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Mamlaka Kamili'.


Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mei 28, 2023.



No comments: