ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 17, 2023

HAKUNA KUFUNGA BIASHARA, ZUNGUMZENI - CHONGOLO



KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM,) Komredi Daniel Chongolo amesisitiza marufuku ya kufunga biashara kama bajeti ilivyopendekeza na kuzitaka mamlaka husika kufanya kazi na wafanyabiashara bila kujenga uadui baina ya Serikali na Taasisi za Serikali na kufanya kazi kwa kuweka mbele mazungumzo, kutafuta suluhu pamoja na kufikia makubaliano.

Chongolo ameyasema hayo Juni 16, 2023 Kibakwe Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya kukagua miradi na utekelezaji wa ilani ya CCM.

"Kulitokea wimbi la watu kila wakiamka asubuhi wanaamua kwenda kufunga biashara ya mtu na wewe unatakiwa kufanya biashara ili upate fedha lakini anakuja anafunga biashara....

Akishafunga biashara anakuja kudai hela,sasa unatoa wapi pesa, ukifunga biashara maana yake umeniambia sina uwezo wa kuja kukulipa hicho unachonidai njia mbadala ni kuweka makubaliano kwamba ikifika tarehe fulani ulipe wewe unaenda kufunga." Amesema.

Amesema, uamuzi huo sio sahihi na ulikuwa unajenga uadui kati ya Serikali au taasisi za Serikali na wafanyabiashara.

"Sasa suala la kufunga biashara halipo,ni kuzungumza na kukubaliana.Bado tumejielekeza huko na maelekezo ya kibajeti ni kwamba ni marufuku sasa biashara kufungwa kwasababu ya jambo lolote linalozungumzika. 

"Tunaipongeza Serikali kwa jambo la msingi sana , kikubwa na mwisho nisisitize bado bajeti hii inajielekeza kuwezesha kutanua wigo wa fursa kwa wananchi." Amesema.

Katibu Mkuu Chongolo yuko kwenye ziara ya siku nane mkoa wa Dodoma akiwa ameambatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC Oganaizesheni Issa Haji Gavu.

No comments: