Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na wadau wakati wa kikao kazi cha kujadili na kupitia maboresho ya Mwongozo wa kupima tija na programu ya kukuza tija na ubunifu nchini kilichofanyika katika jengo la OSHA, jijini Dodoma, Juni 16 2023.
Baadhi ya wadau wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi hicho.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukuzaji Tija, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Yohana Madadi akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili na kupitia maboresho ya Mwongozo wa kupima tija na programu ya kukuza tija na ubunifu nchini kilichofanyika katika jengo la OSHA, jijini Dodoma, Juni 16 2023.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi, amefungua kikao kazi cha kupitia na kujadili rasimu ya mwongozo wa kupima tija na programu ya kukuza tija na ubunifu nchini utakaosaidia kuangalia maendeleo ya ukuaji wa uchumi.
Akifungua kikao hicho Juni 16, 2023 jijini Dodoma, Mhe. Katambi amesema mwongozo huo pia utasaidia kutoa taarifa za namna bora ya kusimamia rasilimali za nchi kwa ufanisi na hivyo kufanya maamuzi sahihi.
Amesema mwongozo huo utatoa dira ya mwelekeo wa namna gani, kwa nini, nini kifanyike na nani afanye nini katika mchakato mzima wa kupima tija.
“Natambua nyaraka nyingine mtakayoijadili ni ya kuhusiana na Programu ya Kukuza Tija na Ubunifu Nchini, hii ni Programu muhimu kwa kuzingatia malengo yake katika kuongeza uelewa wa viwango vya tija na ubunifu katika sekta za umma na binafsi,” amesema
Naibu Waziri Katambi amesema programu hiyo itasaidia kuboresha utendaji, kufanya tafiti, kushauri juu ya ukuaji tija na ubunifu katika sekta mbalimbali na kujenga mfumo madhubuti wa ushirikishwaji na ushiriki wa wadau kwenye utekelezaji, uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa ukuaji wa tija na ubunifu katika sekta za kiuchumi.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukuzaji Tija, Bw. Yohana Madadi ameeleza kuwa kikao kazi hicho kitawezesha kupata maoni ya wadau kuhusu mwongozo huo ambao ni muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Naye, Mhadhiri Chuo cha Mipango Dodoma, Dkt. Erik Ngwega ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuanzisha programu hiyo muhimu ambayo itakuwa chachu kwa vijana kujiajiri wenyewe.
No comments:
Post a Comment