Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othmanakiwasilisha mada tarehe 15 Juni, 2023 katika Mafunzo Elekezi ya Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania yanayomalizika leo tarehe 16 Juni, 2023 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman(aliyekaa katikati), akiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mafunzo Elekezi na Majaji wapya sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania, akiwemo mwingine mmoja ambaye ni Mhe. Jaji Sam Rumanyika (aliyekaa kulia) na (wa pili kulia waliosimama), ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na pia ni Jaji wa Mahakama wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.Dkt. Paul Kihwelo, Mhe. Jaji Zainab Muruke (aliyekaa kushoto). wengine waliosimama (kushoto wa kwanza) ni Mhe. Jaji Leila Mgonya. (wa tatu kulia) ni Mhe. Jaji Amour Khamis, (wa pili kushoto) ni Mhe.Dkt. Jaji Benhajj Masoud, wa (kwanza kulia) ni Mhe. Jaji Gerson Mdemu na (wa tatu kulia) ni Jaji Agnes Mgeyekwa.
Na Mwandishi wetu, Lushoto
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania, kutambua kuwa wananchi wana matumaini makubwa na uteuzi wao, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanakidhi matarajio yao na ya wadau wengine kwenye masuala ya sheria.
Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Othman amesema hayo tarehe 15 Juni, 2023 wakati akiwasilisha mada katika Mafunzo Elekezi ya siku tano kwa Majaji wapya sita wa Mahakama hiyo na mmoja ambaye hakupatiwa mafunzo hapo awali, ambayo yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kilichopo wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Katika wasilisho lake, Mhe. Chande alianza kwa kuwapongeza Majaji hao kwa kuteuliwa kwenda Mahakama ya Rufani, na amewaambia kuwa kuna wadau wengi ukiwemo Umma wa Tanzania ambao una matumaini makubwa juu yao.
"Watu mbalimbali huko nje wana matarajio makubwa na nyie, mtambue hilo, hivyo kafanyeni kazi zenu kwa uadilifu, jamii inawasubirini kwa hamu, maana nyie ni wapya," amesema Jaji Mkuu Mstaafu Othman.
Aidha amewaambia Majaji hao kuwa wana majukumu mazito mbele yao, na kwamba ni wajibu wao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na umakini mkubwa.
Vile vile, Mhe. Othman amewataka Majaji hao kutumikia majukumu yao mapya ya Mahakama hiyo katika namna itakayowafanya waache urithi mzuri kwa jamii.
"Mnatakiwa kuacha urithi(Legacy) katika Mahakama ya Rufani. Urithi katika maeneo mbalimbali, mathalani Jaji Mstaafu Mhe. Lewis Makame alikuwa akiandika hukumu zake kwa mtindo wa mashairi, uzuri yeye alisoma Kiingereza na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Makerere," amesisitiza. Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Othman.
Mada ya kwanza ya Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Chande ilizungumzia kipindi cha Mpito, matarajio, majukumu na matumaini ya umma na ilikuwa na maudhui yanayosema "Mabadiliko kwenda Mahakama ya juu: Ujaji wa Rufaa kama kazi ya hadhi ya juu (Transition to the Higher Bench: Justice of Appeal as an Advance Career).
Kwa upande mwingine Jaji Mkuu Mstaafu Chande amewahimiza Majaji hao kufanya kazi kwa kushirikiana ili kupata matokeo bora ya kazi.
"Tufanye kazi kwa pamoja, kila mmoja kaingia kwa bahati yake, uwezo wake na kipaji chake, hakuna mashindano, kwa kufanya hivyo, kazi inakuwa rahisi," amesema.
Mhe. Jaji Othman aliwasilisha mada yake ya pili iliyokuwa na maudhui Ushirikiano katika Mahakama ya Rufani (Collegiality at the Court of Appeal).
Majaji wapya sita (6) wanaopatiwa mafunzo hayo ni wale waliyoteuliwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 28 Aprili, 2023 na kuapishwa tarehe 23 Mei, 2023 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Nao washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Jaji mpya wa Mahakama ya Rufani, Tanzania, Mhe. Amour Said Khamis amesema kuwa mada ya Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Othman imesaidia kutambua changamoto na kazi iliyopo mbele yao kwenye Mahakama hiyo.
Kwa upande wake, Jaji mpya wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Agnes Mgeyekwa amesema kuwa mada hiyo imewajengea hali ya kujiamini na jinsi ya kukabiliana na mashinikizo ya watu katika utekelezaji wa kazi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa tarehe 12 Juni, 2023 na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma na yanamalizika leo tarehe 16 Juni, 2023.
Majaji wanaopatiwa mafunzo hayo ni Mhe. Jaji Sam Mpaya Rumanyika, Mhe. Jaji Zainab Muruke, Mhe. Jaji Leila Mgonya, Mhe. Jaji Amour Khamis, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud, Mhe. Gerson Mdemu na Mhe. Jaji Agnes Mgeyekwa.
Aidha Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
No comments:
Post a Comment