Sunday, January 28, 2024

JUMLA YA VIFO 2,648 VITOKANAVYO NA UZAZI VYAZUILIKA KWENYE MIKOA 10 NCHINI



Mkurugenzi mtendaji wa UMAT,Bi Suzana Mkanzabi akitoa taarfa ya mradi wa WISH 2 ACTION katika mkutano na wadau wa Afya ya Uzazi.

Jumla ya vifo 2,648 vinavyotokana na uzazi vimeweza kuzuiwa katika mikoa 10 nchini huku serikali ikiendelea na mikakati kudhibiti matukio ya utoaji mimba wakati takwimu zikionesha mpaka sasa kuna matukio 458,139 ya utoaji mimba usio salama.

Kupitia mradi wa WISH 2 ACTION wenye lengo la kuchochea mabadiliko ya afya ya uzazi, serikali imefanikiwa kuepusha mimba zisizotarajiwa zaidi ya mimba milioni 1.6 katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma,Mara,Rukwa,Ruvuma Njombe, katavi na Mbeya.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UMATI Suzana Mkanzabi, wakati alipowakutanisha wadau wote waliofanikisha utekelezaji wa mradi huo, kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza.

Alisema kuwa jumla ya watu milioni 3.8 wamepatiwa huduma za afya ya uzazi na vituo vya afya takribani 300 vimepatiwa vifaa tiba kupitia mradi huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Shirika la Marie Stopes Dk Geofrey Sigalla alisema mradi huo umelenga kumkomboa mwananchi hasa anaetoka kaya maskini katika maeneo ya uzazi wa mpango, maambukizi ya Ukimwi na kukinga saratani ya kizazi kwa wanawake.

Pamoja na mambo mengine Dk Sigalla aliiomba serikali kujikita katika kutatua changamoto maeneo mtambuka ikiwemo kuwezesha vituo vya afya kutoa huduma himilivu kama vile kuongeza vitendea kazi, pamoja na kuwa na uwezo wa kuwafikia wateja.

Mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Yahya Hussein alisema mradi wa kutoa elimu ya afya ya uzazi utaendelezwa na serikali kutokana na mafanikio yake.

Tanzania kama nchi zingine duniani inatekeleza Malengo endelevu wa Dunia SDGs inayotaka kila nchi mwanachama kupunguza vifo vitokavyo na uzazi kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000

No comments: