Sunday, January 28, 2024

POLISI TANGA WAMNASA ALIYEMTEKA MTOTO WA MIAKA MITATU ILI APEWE MILIONI 1.5 NDIO AMUACHIE HURU


Na Raisa Said, Tanga

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kumuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 3 aliyetekwa na mtu asiyejulikana ambapo baada ya kumteka alitaka apatiwe Sh.milioni 1.5 ili amuaache huru.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamisha Msaidizi wa Polisi Almachius Mchunguzi amesema Januari 23 mwaka huu saa 10 jioni jeshi hilo kupitia vyanzo vyake lilipokea taarifa ya tukio hilo la kutekwa kwa mtoto huyo eneo la Mji Mpya Wilayani Korogwe.

Amesema mtoto huyo alitekwa alipokuwa akitoka kucheza katika nyumba ya jirani , hivyo baada ya tukio hilo Januari 25 mwaka huu katika kitongoji cha Sagama 'A' kijiji cha kwamkono, Tarafa ya Sindeo wilayani Handeni jeshi hilo lilifanya msako na kufanikiwa kumtia mbaroni Ramadhani Adinai Mbano (21)mkazi wa Manundu Korogwe akiwa na mtoto huyo.

Kamanda Mchunguzi amesema kwa sasa taratibu nyingine za kisheria zinakamilishwa ili mtuhumiwa huyo afikishwe nahakamani sheria ichukue mkondo wake huku mtoto akipelekwa kwa wataalamu wa afya kwa uchunguzi na taratibu za kumrejesha kwa mama yake zikifanyika

Ametoa mwito kwa wazazi/walezi wawalinde watoto wao kwa karibu ili kuwaepusha na vitendo vya watu wenye nia ovu kama vile utekaji,ubakaji na ulawiti kutokupata nafasi.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mji wa Korogwe Judith Kazimoto amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea wilayani hapo ingawa matukio ya ukatili dhidi ya watoto yapo kwa wingi wilayani humo.

Amesema wanapata kesi kati ya tatu hadi nne kwa mwezi na akayataja matukio yaliyoshamiri kuwa ni ubakaji na ulawiti kwa watoto wenye umri wa miaka nane kwenda chini.

Hata hivyo alitaja changamoto ya wazazi na walezi kuyamaliza matatizo hayo nyumbani kwa sababu wahusika mara nyingi wanakuwa ndugu na jamaa wa karibu na familia.

Ametoa mwito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuacha kuwalinda wahalifu na wakubali kuwafikisha mbele ya sheria ili kukomesha ukatili huo.

No comments: