Wednesday, January 24, 2024

SAFARI YA INDONESIA YA RAIS SAMIA SIKU AMBAYO CHADEMA WANAANDAMANA YAZUA GUMZO KILA PEMBE


Kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kuanza safari ya nje ya nchi wakati chama kikuu cha upinzani kikiwa kwenye maandamano kimeelezwa kuwa ni cha kishujaa na cha kujiamini kupita kiasi.


Wengi tuliowahoji wamesema Rais Samia ameonesha ukomavu wa hali ya juu kwa kuruhusu maandamano yaendelee huku yeye mwenyewe akijiandaa kuondoka nchini kuelekea Indonesia kama hakuna kitu kinachotokea.

 

Hivyo ndivyo Rais Samia asivyokuwa na shaka juu ya mustakabali wa amani na usalama nchini, na anaviamini mno vyombo vyake vya dola, walisema. 


Kwenye mitandao ya kijamii ndio usiseme. Mjadala huo umepamba moto kiasi maandamano yanaonekana kukosa mvuto kabisa.

 

“Hii inataka ujasiri wa hali ya juu na kujiamini sana”, Jacob Tendewe amesema, akiongezea kwamba kwa nchi zingine vyama vya upinzani vikikohoa tu Rais huwa hatoki hata Ikulu. Ona huyu mama anaenda safari ya mbali hivyo bila wasiwasi.

 

Wengine wamekifananisha kitendo cha Rais Samia kuondoka Tanzania na kwenda katika ziara ya nje ya bara la Afrika ni kofi aina ya ‘kelb’ alichowachapa nalo CHADEMA, akimaanisha hawana ubavu wala ujanja wa kufanya jambo lolote zaidi ya kubwabwaja tu.

 

“Mimi ningekuwa CHADEMA ningeitisha maandamano mengine kupinga kwa nini mama aondoke nchini siku ambayo sisi tunaandamana. 

 

“Yaani ina maana Mama Samia hauogopi upinzani na ameudharau kiasi hicho kweli?”, amesema Bi Rukia Maneno wa Dar es salaam.

 

Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kwamba safari hiyo ilikuwa imepangwa tokea muda mrefu uliopita, na kwamba inaenda sambamba na mipango ya kumpokea Rais wa Indonesia miezi michache ijayo.

 

“Kupanga na kuitekeleza safari ya kiongozi mkuu kama Rais sio jambo dogo na lina gharama zake hasa hasa unapoahirisha.

 

“Rais anaweza kuahirisha safari kwa sababu nzito kama janga la kitaifa kama alivyofanya kufuatia mafuriko kule Hanang.

 

“Lakini kuahirisha kwa sababu ya maandamano ya chama cha upinzani haiingii akilini kwa sababu hilo jambo bila shaka halina uzito wa kitaifa kiasi hicho.

 

Na ukiona hivyo vyombo vimemhakikishia Mama amani na usalama wa kutosha awepo ama asiwepo”, kimesema Chanzo kimoja toka sehemu nyeti.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Soekarno-Hatta, Tangerang kwa ajili ya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia tarehe leo 24 Januari, 2024.


 

No comments: