Friday, January 26, 2024

WAZIRI NAPE AIPA SIKU 7 NHC KUTOA TAARIFA YA KUKAMILIKA KWA UJENZI WA JENGO LA WIZARA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amelitaka Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) kuwasilisha maelezo ndani ya siku saba kueleza ni lini watakamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi za wizara hiyo lililopo Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma.

Waziri Nape ameyasema hayo leo tarehe 24 Januari, 2024 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara hiyo. Katika ukaguzi, Mhe. Nape amekagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo zima sambamba na kukagua vifaa vya ujenzi ambavyo tayari vimeshanunuliwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Jengo zima.
Naye Mhandisi Peter Mwaisabula ambaye ni Meneja Mradi kutoka Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) amemuhakikishia Waziri Nape kuwa ifikapo mwezi Mei, 2024 Jengo la Ofisi za wizara litakuwa limekamilika kwa kuwa vifaa vingi vinavyohitajika kukamilisha ujenzi huo vipo. Katika ziara hii, Waziri Nape aliambatana na Viongozi wa Menejimenti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiongozwa na Karibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Mohammed Khamis Abdulla.




No comments: