Thursday, February 1, 2024

BALOZI MBAROUK APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KUTOKA KWA BALOZI MTEULE WA BURUNDI


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akipokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mhe. Leontine Nzeyimana wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amepokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Leontine Nzeyimana.

Akipokea Nakala hizo Mhe. Mabarouk amemuhakikishia Mhe. Nzeyimana ushirikiano wa dhati utakaomwezesha kuitumikia Burundi kwa tija katika muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Vilevile, alieleza kuwa Tanzania na Burundi licha ya kuwa na ushirikiano wa ujirani pia ni ndugu kufuatia mwingiliano wa wananchi wa Nchi hizi mbili hususan kwenye masuala ya biashara.

“Tanzania itaendelea kuweka mikakati imara ya kukuza ushirikiano wa kibiashara sambamba na kusimamia ujenzi wa miundombinu inayounganisha nchi hizo ili kurahisisha shughuli za usafirishaji”. Mhe. Balozi Mbarouk

Naye Balozi Mteule, Mhe. Leontine Nzeyimana alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata tangu alipowasili nchini na kwamba ana matumaini makubwa ya kupata ushirikiano utakaomwezesha kutekeleza majukumu yake ya uwakilishi kikamilifu.

Viongozi hao pia wamekubaliana kuendelea kuratibu utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa na Nchi zao kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ili kuleta tija kwa pande zote.

Pamoja na mambo mengine, kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Burundi nchini, Mhe. Evaristi Ndayishimye Tanzania ilikabidhi eneo la bandari kavu katika eneo la Kwala mkoani Pwani ili kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.
Asilimia 75 ya mizigo ya Burundi husafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam hivyo, bandari kavu ni chachu kubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

No comments: