Friday, February 2, 2024

MAJALIWA AMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MKUTANO WA DHARURA WA SADC


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa dharura wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Angola, Joao Manuel Lourenco ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, ulikuwa na ajenda moja tu ya kujadili kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika ukanda wa SADC.

Akizungumza kutoka ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma leo (Ijumaa, Februari 02, 2024), Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania inapendekeza kuwa ni vema Kanda ya SADC ikachukua hatua jumuishi kwa kuhusisha sekta zote mtambuka ikiwemo sekta za maji na mipango miji ili kuleta suluhisho la kudumu la kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko.

“Hii ni kwa kuzingatia kuwa jamii kwa ujumla na kila mwananchi ana jukumu la kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha anazingatia kanuni za usafi (WASH) kwa manufaa binafsi, jamii na ukanda mzima.”

“Tunashauri nguvu kubwa ielekezwe katika kuboresha mifumo na upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii zetu ili kuwa na matokeo chanya katika kudhibiti mlipuko huu.”

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu; Waziri wa Maji, Jumaa Aweso pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

Mapema, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa SADC, Rais Lourenco alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha mawasiliano baina ya wataalamu wake ili kusaidiana kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hasa kwenye maeneo ya mipakani.

Aidha, alisisitiza viongozi wa nchi wanachama waweke kipaumbele kwenye teknolojia mpya na tafiti ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. “Ni lazima tuhakikishe mifumo yetu ya afya inaweza kukabili na changamoto hizi za magonjwa ya mlipuko.”

Marais walioshiriki mkutano huo ni Phillipe Nyusi (Msumbiji), Lazarus Chikwera (Malawi), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Haikande Hichelema (Zambia) Felix Tshisekedi (DRC). Wengine ni wawakilishi wa Wakuu wa Nchi kutoka Afrika Kusini, Lesotho, Eswatini, Seychelles na Madagascar.

No comments: